Habari MsetoSiasa

Seneti yatoa Sh200m kupiga vita corona

March 31st, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

BUNGE la Seneti limetoa Sh200 milioni kutoka kwa bajeti yake ya mwaka wa kifedha wa 2019/2020 kupiga jeki mpango wa kupambana na kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19.

Spika wa Bunge hilo Ken Lusaka, alitoa tangazo hilo jana alasiri maseneta waliporejelea vikao baada ya mapumziko ya majuma mawili.

Bw Lusaka alisema maseneta wamekubaliana na hatua hiyo kwa kauli moja kama sehemu ya kusaidia juhudi za serikali za kudhibiti janga hilo.

“Kwa hivyo, seneti inaiomba Tume ya Huduma za Bunge (PSC) kutekeleza hatua ya kupunguza kiasi cha Sh200 milioni kutoka bajeti yake ya mwaka huu wa kifedha. PSC iwasiliane na Hazina ya Kitaifa ili pesa hizo zielekezwe kwa mpango wa kupambana na janga hilo la Covid-19,” Bw Lusaka akasema.

Jana, maseneta walirejelea vikao ambapo janga la Covid-19 lilijadiliwa kwa kina. Ni maseneta 28 pekee walioruhusiwa katika Seneti ili kudumisha hitaji la kutokaribiana.

Seneta wa Nairobi, Bw Johnson Sakaja alipendekeza pesa zilizotengewa idara mbalimbali zirudishwe kwa hazina ya kutoa misaada kwa wananchi wakati huu wanapotaabika kwa janga la corona.

“Haina maana kusema mabilioni ya pesa zimetengewa miradi ya miundomsingi kama hatuwezi kulisha wananchi wetu,” akasema Bw Sakaja.

Bunge la Kitaifa litafanya kikao maalumu mnamo Jumatano wiki ujao kupitisha mswada wa kufanikisha mpango wa serikali wa kupunguza athari za mkurupuko wa virusi vya corona kwa wananchi na uchumi kwa ujumla.

Kwenye ombi alilowasilisha kwa Spika Justin Muturi, kiongozi wa wengi Aden Duale anasema wabunge pia watajadili na kupitisha bajeti ya ziada na kanuni za kufanikisha utendakazi wa Hazina ya Dharura ya kukabilia na makali ya ugonjwa wa Covid-19.

Wabunge wanatarajiwa kupitisha Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Ushuru, 2020 ambao utatekeleza miongoni mwa mapendekezo yaliyotangazwa na Rais Uhuru Kenyatta wiki jana kama vile kufutuliwa mbali kwa aina zote za ushuru kwa wafanyakazi wanaopokea mshahara usiozidi Sh24,000 kwa mwezi.