Habari Mseto

Seneti yatofautiana na serikali kuhusu kiini cha uchomaji wa shule

July 18th, 2018 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MATUMIZI ya mihadarati, ukosefu wa malezi bora, na usimamizi mbaya ni miongoni mwa sababu ambazo zinachangia kukithiri kwa visa vya utovu wa nidhamu na uteketaji wa majengo ya shule, maseneta wamesema.

Viongozi hao ambao ni wanachama wa Kamati ya Seneti kuhusu Elimu Jumatano walisema visa hivyo havisababishwi na hofu ya mitihani ya kitaifa, ilivyoelezwa na Wizara ya Elimu.

“Fujo na visa vya wanafunzi kuteketeza shule za sasa zimegeuka kuwa kero kubwa nchini. Katika siku kadha zilizopita mali ya thamani kubwa imeharibiwa katika shule kadha nchini baada ya wanafunzi kuteketeza mabweni na majengo mengine shuleni.

Suala hilo sasa linapasa kushughulikiwa kwa makini,” mwenyekiti wa kamati hiyo Seneta Andrew Langat akasema kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge.

Aliandama na wanachama wengine wa kamati hiyo maseneta; Profesa Sam Ongeri (Kisii), John Kinyua (Laikipia) na maseneta maalum Rose Nyamunga na Mary Seneta.

Bw Lang’at ambaye ni seneta wa Bomet aliongeza kuwa wadau katika sekta ya elimu wanapaswa kujadili njia za kumaliza shida ya matumizi ya dawa za kulevya shuleni haswa katika shule za upili za mabweni

“Juzi nilitembelea shule ya upili ya Sunshine iliyoko kaunti ya Nairobi na kukumbana na kisa ambapo walinzi waliwakamata watu fulani ambao walikuwa wakipanga kuingiza mihadarati katika shule hii. Hii ni ithibati kuwa matumizi ya dawa hizo ni mojawapo wa sasa ya visa utovu wa nidhamu katika shule zetu,” akasema.

Bw Langat pia aliitaka wizara ya elimu kutengea shule za upili pesa za kufadhili kubuniwa kwa idara za kutoa ushauri nasaha katika shule zote humu nchini.

Profesa Ongeri ambaye aliwahi kuhudumu kama Waziri wa Elimu, alisema mabadiliko katika tamadumi za jamii mbali mbali zimechangia kidorora kwa maadili, hali ambayo imeathiri wanafunzi haswa walio katika umri wa kubaleghe.?

“Hili ni tatizo kubwa ambalo linafaa kutafutiwa ufumbuzi kwa sababu vichocheo vya hali hii hubadilika mwaka baada ya mwaka. Hii ndio maana kero hili linafaa kujadiliwa katika jukwaa moja kitaifa,” akasema.

Kufikia sasa zaidi ya shule 30 zimefungwa baada ya wanafunzi kuzua fujo na kuteketeza baadhi yazo. Shule ya hivi punde kufungwa kutokana na kisa cha moto ni Shule ya Upili ya Kitaifa ya Kisii School.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut) Wilson Sossion amewataka wanafunzi kubuni njia mbadala za kushughulia matatizo yao shule badala ya kuchoma shule.