Habari

Seneti yazimwa kumjadili Samboja

October 17th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

BUNGE la Seneti limezimwa na Mahakama Kuu kujadili hoja ya kumwondoa mamlakani Gavana wa Taita Taveta Granton Samboja.

Jaji Weldon Korir ameiamuru Seneti ikome kujadili hoja hiyo ya kumwondoa Gavana Samboja hadi kesi aliyowasilisha kinara huyo wa kaunti isikizwe na kuamuliwa.

Jaji Korir aliratibisha kuwa ya dharura kesi aliyowasilisha Bw Samboja kupitia kwa wakili Nelson Havi.

Jaji huyo alisema masuala ya kisheria aliyozua Bw Samboja yanahitaji kuamuliwa baada ya washtakiwa kuwasilisha ushahidi.

“Kuna masuala muhimu ya kisheria na kikatiba ambayo Bw Samboja anaomba mahakama kuamua iwapo madiwani walizingatia sheria walipojadili hoja ya kumtimua kazini,” amesema Jaji Korir.

Mbali na kulizuia bunge lote la Seneti kujadili hoja ya kutimuliwa kwa Bw Samboja, Jaji Korir pia amezuia kamati za Seneti na pia bunge la kaunti ya Taita Taveta kujadilia suala hilo la kumkomoa mamlakani hadi kesi iliyowasilishwa mahakamani kusikizwa na kuamuliwa.

Gavana huyo aliwasilisha kesi dhidi ya Serikali ya Kaunti ya Taita Taveta, Spika wa bunge la Kaunti ya Taita Taveta, Bunge la Seneti, Mheshimiwa Harris Keke na Spika wa Seneti Kenneth Lusaka.

Mnamo Oktoba 11, 2019, Bw Samboja aliwasilisha kesi hiyo katika mahakama kuu akisema haki zake zimekandamizwa na uamuzi wa madiwani kumfuta kwa madai ya utovu wa nidhamu.

Madiwani hao walidai katika ushahidi wao kwamba, Bw Samboja hakuwa anatekeleza majukumu yake ipasavyo na kwa mujibu wa kisheria.

Katika mawasilisho yake, Bw Samboja amedai haki zake zilikandamizwa na uamuzi huo wa madiwani kumkomoa mamlakani.

Jaji Korir ameamuru kesi isikizwe Oktoba 28, 2019.