Habari Mseto

SENSA 2019: Idara yaanzisha majaribio

August 27th, 2018 2 min read

Na COLLINS OMULO

HALMASHAURI ya Kitaifa ya Ukusanyaji Takwimu (KNBS) imeanza majaribio ya kukusanya habari muhimu kwa wananchi kama matayarisho ya sensa inayopangiwa kufanyika Agosti, 2019.

Zoezi hilo, ambalo lilianza Agosti 25, linatarajiwa kufanyika katika kaunti 12, huku likimalizika Agosti 31. Kaunti hizo ni pamoja na Nairobi, Kwale, Kilifi, Makueni, Nyeri, Tharaka Nithi, Mandera, Pokot Magharibi, Kericho, Busia, Kisumu na Kisii.

Mkururenzi Mkuu wa halmashauri hiyo, Bw Zachary Mwangi, alisema shughuli hiyo itaendeshwa katika maeneo maalum ambayo tayari yashabainishwa.

Alieleza kuwa lengo lake kuu ni kuwafahamisha wananchi kuhusu maelezo muhimu ambayo watatakiwa kutoa kuwahusu shughuli hiyo itakapoanza rasmi.

“Majaribio ya shughuli hii yanapaswa kufanyika mwaka mmoja kabla ya zoezi rasmi kuanza. Litakuchukua muda wa siku saba. Tuna watu 380 ambao watashiriki moja kwa moja katika zoezi la uhesabu, wasimamizi 71 na washirikishi kadhaa,” akasema Bw Mwangi, kwenye uzinduzi wa zoezi hilo katika eneo la Imara Daima, Nairobi.

Sensa hiyo imepangiwa kugharimu Sh18.5 bilioni. Kati ya fedha hizo, Sh3.5 bilioni zitatumika kununulia simu 164,000 za kisasa na vifaa vingine vya kimitambo. Kiasi kitakachobaki kitatumika kuwalipia zaidi ya makarani 190,000 watakaoshiriki katika uhesabu wa watu.

Alipofika mbele ya Kamati ya Bunge Kuhusu Mageuzi ya Katiba mnamo Februari mwaka huu, Bw Mwangi aliiambia kamati hiyo kwamba, takwimu za mwanzo kuhusu sensa hiyo zitatolewa katika muda wa mwezi mmoja. Hata hivyo, ripoti kamili kuhusu idadi kamili ya watu itatolewa kufikia Juni 2020.

Kulingana na Bw Mwangi, majaribio hayo yatatathmini umahsusi wa vifaa muhimu kama simu, fomu, zoezi la kujumuisha masuala mbalimbali kati ya mengine muhimu.

Vifaa vingine vilivyotathminiwa ni ramani, utaratibu wa kuweka data, na uthibitishaji wa viwango vya imani ya zoezi hilo miongoni mwa wananchi.

“Zoezi hilo hutusaidia kutathmini ufaafu wa maswali tutakayowauliza wananchi, wakati wa kuyauliza, utaratibu tutakaofuata na ufahamu wa changamoto tutakazokumbana nazo,” akasema.

Kenya imekuwa ikifanya zoezi hilo kila baada ya miaka kumi tangu 1969.

Katika matayarisho ya zoezi hilo, halmashauri hiyo imebaini kaunti 28 ambapo majaribio hayo yataendelea, hata baada ya muda kamili wa shughuli husika kukamilika mnamo Agosti 31.

“Tulianza zoezi hili miaka mitatu iliyopita ambapo tumefikia maeneo mengi sana. Tumebaini kaunti 28 ambazo tutaliendeleza,” akasema.

Sensa ya mwisho ilifanyika mnamo 2009, ambapo Kenya ilibainika kuwa na watu milioni 38. Hilo lilikuwa ongezeko la watu milioni 10, kutoka watu 28.7 milioni kwenye sensa ya 1999.

Shughuli ya kuhesabu watu hufanywa kila baada ya miaka kumi. Lengo la kujua idadi kamili ya watu ni kuiwezesha serikali kufanyia mageuzi baadhi ya mipango yake ya maendeleo, ili kukidhi mahitaji ya idadi ya wananchi waliopo.

Pia, hutumiwa na Tume Huru ya Uchaguzi kuangalia upya maeneo ya uwakilishi, kama yaongezwe, yaunganishwe au yapunguzwe.