Makala

SENSA: Hofu ya wanasiasa Mlima Kenya

September 11th, 2019 3 min read

Na MWANGI MUIRURI

HAIJULIKANI hasa ni kwa msingi gani ambapo wanasiasa wengi wa Mlima Kenya hukesha wakilalamika kuwa “idadi zetu – jamii za Gema (ushirika wa Gikuyu, Embu na Ameru) – zinapungua kila uchao.”

Ingawa wanasiasa wengi katika eneo hilo huwa na kati ya watoto wawili na watatu katika ndoa zao au ulezi wao, bila kuzingatia wa nje ya ndoa, wao husukuma kampeni kali wakiwataka wenyeji wazaane.

Ni hali mbaya kiuchumi kuwataka raia wa kipato cha chini wazae kwa sababu tu za kisiasa bali sio kwa msingi wa uwezo wa malezi.

Siasa ni mchezo mchafu.

Hata somo la sayansi ya siasa lililemewa na kuipa maana dhana ya “siasa” na ikaafikiana kuwa “sisi wote ni wanasiasa katika hali zetu zote za kimaisha.”

Ni kauli anayopenda kutumia mhadhiri Gasper Odhiambo.

Ni katika hali hiyo ambapo Seneta wa Kiambu, Kimani wa Matangi alisema anaomba Mungu sensa ya mwaka 2019 isije ikathibitisha huenda “tumepitwa kwa idadi na jamii kama ya Akamba na Abaluhya.”

Analia kuwa katika eneo la Mlima Kenya, kumekuwa na maandamano tele ya wanawake wakiteta kuhusu kupotea kwa nguvu za kiume miongoni mwa wanaume wa eneo hilo hivyo basi kupunguza uwezo wa kuzaa.

Aidha, mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria anateta kuwa ulevi umekuwa tisho kuu kwa wenyeji.

“Hapa kwetu shule za msingi zinafungwa kwa kukosa watoto wa kusajiliwa kama wanafunzi,” akasema Kuria.

Anasema kuwa ulevi huo pamoja na utumizi wa dawa za kupanga uzazi miongoni mwa wanawake wa eneo hilo kumesababisha kukosa kuafikia malengo ya kuongezeka kwa takriban watu milioni moja kwa mwaka.

Gavana wa Nyandarua, Francis Kimemia anasema kuwa hesabu ya watu na nyumba iliyofanywa 2009  ilionyesha upungufu wa watu 1.8 Milioni kwa kuwa ilitarajiwa wafike  zaidi ya Millioni nane lakini wakawa 6.3 milioni.

“Tukaze tukiomba sensa hii ya sasa itupe matumaini ya kesho yetu katika siasa,” asema.

Ni hali ambayo imewaelekeza wengine wa wanasiasa wa eneo hilo kutangaza zawadi za pesa taslimu kwa walevi wote ambao watatema uraibu wao na watunge wanawake wao mimba, zawadi hiyo ikiwa kati ya Sh500 na Sh1,000!

Aidha, Bw Kimemia alidai kuwa pombe haramu zilielekezwa katika jamii hizo miaka ya 80 kwa misingi ya siasa ambapo nia ilikuwa kuwamaliza kizazi.

“Ni lazima watu wa jamii hizi wajiulize mbona ni kwao tu pombe hizi zilikubaliwa ziuzwe bila ya kuthibitiwa. Na tangu maeneo yenu yafanywe kuwa kiwanda na pia soko ya pombe hizi, hamuzai na serikali inaashiria kuunganisha baadhi ya mashule kwani mengi hayana idadi ya kuhudumiwa na walimu 10,” akasema.

Katika hali hiyo, wanawake wa eneo hilo wameshawishiwa walegeze kinga dhidi ya kupata uja uzito kupitia utumiaji dawa za kupanga uzazi na washirikiane na waume zao ili kupambana na upungufu wa watoto katika eneo hilo.

Mshirikishi wa kitaifa wa Shirika la Wanawake Waelimishaji (Fawe) Bi Cecilia Gitu anasema kuwa utumiaji wa dawa za kupanga uzazi bila ya kuwahusisha waume zao unasababisha upungufu wa watoto katika eneo hilo.

Alisema idadi ya watoto wanaozaliwa kila mwezi eneo hilo imepungua hadi wane kwa sasa ikilinganishwa na watoto saba waliokuwa wakizaliwa mwaka wa 1998.

Ripoti ya Shirika la Kenya Demographic Health Survey (KDHS) 2018 ilionyesha kuwa asilimia 67 ya wanawake wa Mlima Kenya hutumia dawa za kupanga uzazi na huwa hawaelezei waume zao kuhusu hali hiyo.

“Ukiambatanisha na idadi ya wazee wanaokunywa pombe kupindukia hivyo basi kulemewa na majukumu muhimu ya ndoa, utaona hali ya hatari kuhusu vizazi vijavyo kwani idadi yao itakuwa chache mno,” akasema.

Alilalamika kuwa kwa sasa hospitali nyingi hata hazipati waja wazito wa kuhudumia na shule nyingi za nasari imefungwa kwa kukosa watoto wa kusajili.

“Nyakati tulikuwa tunasikia shule moja ya msingi iko na watoto zaidi ya 2,000 zimeisha na sasa hata serikali inawaza kujumuisha shule kadhaa pamoja kwani hakuna idadi ya kufundishwa na walimu zaidi ya 10,” akateta.