Habari MsetoSiasa

SENSA: Idadi kubwa ya Wakenya huishi Rift Valley na Mlima Kenya

November 5th, 2019 2 min read

Na JUMA NAMLOLA

ENEO la Rift Valley limo kifua mbele kupata mgao mkubwa wa maendeleo na usemi wa kisiasa baada ya kuandikisha idadi kubwa zaidi ya watu kwenye sensa iliyofanyika Agosti.

Kulingana na matokeo hayo, Rift Valley inaongoza kwa watu 12,442,639 wanaotoka kaunti 13. Idadi hii ni robo ya Wakenya wote.

Eneo la Mlima Kenya linafuata kwa jumla ya watu 8,029,729 wengi wao wakiwa wa kutoka Kiambu (2,417,735), huku wachache zaidi wakitoka Kaunti ya Tharaka Nithi (393,177).

Tayari viongozi wa Tharaka Nithi, ambayo wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2007 ilidhaniwa kuwa na wapiga kura wengi zaidi nchini, wamelalama na kuapa kwenda kortini iwapo Baraza la Takwimu Nchini (KNBS) halitahesabu upya watu wake.

Nyanza ikiwa na watu 6,269,579 ni ya tatu ikifuatwa na Magharibi (5,021,843), Nairobi (4,397,073), Pwani (4,329,474) na Ukambani (3,545,772).

Maeneo ya jamii za wafugaji katika uliokuwa mkoa wa Mashariki pamoja na wenzao wa kaunti tatu za Kaskazini Mashariki, wanafikia idadi ya watu 3,528,187.

Katika siku za majuzi viongozi wa Mlima Kenya wamekuwa wakisisitiza mfumo wa ugawaji raslimali za nchi ufanywe kulingana na idadi ya watu badala ya ukubwa wa eneo.

Viongozi wanasema watakataa ripoti ya Jopo ya Maridhiano (BBI) iwapo haitaangazia maeneo yao ya uwakilishi.

Eneo hilo ambalo kwa miaka mingi limekuwa na uwakilishi serikalini, hasa katika ngazi ya urais, linataka BBI ipendekeze kugawanywa na kusambazwa kwa maendeleo kulingana na idadi ya watu.

Waziri wa Kilimo, Bw Mwangi Kiunjuri amekuwa mstari wa mbele kuwataka watu wa eneo hilo wakatae BBI kwa misingi kuwa itawapa watu walio na idadi ndogo uwezo sawa na wao katika maamuzi muhimu ya kitaifa.

Ijapokuwa kimsingi Laikipia anakotoka Bw Kiunjuri ipo Rift Valley, anaamini iwapo kila kura itaheshimiwa, basi watu wa Mlima Kenya watapata manufaa ya mageuzi ya Katiba yanayotarajiwa.

Wadadisi wa masuala ya siasa na uchumi wanahisi kuwa iwapo mfumo wa idadi ya watu utatumiwa kama kigezo cha kupeleka maendeleo, watu walio maeneo yaliyotengwa wataendelea kubaki nyuma kwa miaka mingi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Pwani, Profesa Halim Shauri anaamini kuwa mbali na idadi ya watu, ukubwa wa maeneo wafaa kuzingatiwa.

“Pendekezo la kugawa maeneo bunge kuwa mengi zaidi halina mashiko. Kinachofaa kuangaliwa ni iwapo uchumi wa nchi yetu unaweza kuhimili uzito wa mahitaji yetu ya kifedha,” anasema Prof Shauri.

Kwa msingi huo, anapendekeza kwamba mfumo bora zaidi wafaa kuwa ule ya kuyagawa maeneo kwa kuzingatia idadi ya watu hasa kwa wastani wa kati ya milioni 3 na 4 ili kuwe na maeneo yasiyozidi 15.