Habari Mseto

SENSA: Kuna wakulima milioni 6.4 pekee nchini

March 3rd, 2020 2 min read

Na DIANA MUTHEU

Kilimo ndio uti wa mgongo wa taifa letu lakini kulingana na ripoti moja, kati ya watu milioni 47.9  nchini, ni milioni 6.4 pekee ambao ni wakulima.

Kulingana na matokeo ya Sensa ya 2019, mimea maarufu inayopandwa nchini ni mahindi na maharagwe.

“Watu 5.1 milioni walijihusisha na kilimo cha mahindi na wengine 3.6 milioni walipanda maharagwe,” ikasema ripoti.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Sensa iliyoandaliwa na Shirika la Takwimu Nchini (KNBS), watu 4.7 milioni walifuga wanyama.

Akizungumza na Taifa Leo, Naibu Waziri wa Kilimo Prof Hamadi Boga alisema asilimia 60 ya wakulima nchini hupanda mahindi na maharagwe kwa kuwa watu wengi nchini hula bidhaa za mahindi kama vile ugali na Githeri.

“Kila wakati nchi inapokua, watu wachache hujihusisha moja kwa moja na kilimo shambani kwa kuwa hali ya maisha hubadilika, majengo mapya yakajengwa na watu wakahamia katika miji mikubwa.

“Tunahitaji wakulima wachache ambao watapanda mimea katika vipande vikubwa vya ardhi na wengine wajiunge na sekta ya kuboresha vyakula,” akasema Prof Boga.

Naibu waziri huyu alisema kuwa tatizo kubwa ni kuhakikisha kuwa nchi inapata mazao ya kutosha.

“Umri wa wastani wa mkulima ni 51 kwa kuwa wengi wana shamba na uwezo wa kulima. Vijana wengi uhamia katika miji mikubwa ambapo hawajihusishi na kilimo cha moja kwa moja ilhali wao ni asilimia 75 ya watu wote nchini,” akasema naibu waziri.

Katika sekta ya samaki, ripoti hii ilisema kuwa familia 109,640 ilijihusisha na uvuvi. Ufugaji wa samaki ulionekana kuwa wa chini sana huku watu 29,325 pekee wakijihusisha nao.

Prof Boga alisema jamii zingine hapo awali zilidhania samaki ni aina ya nyoka lakini walipofunzwa, wakajua ni chakula bora.

“Wakenya wengi hawali samaki sana lakini wameanza kujifunza. Kampeni za kuhamasisha watu kula samaki zitaendelea kwa kuwa ni chakula ambacho kina protini ya kutosha,” akasema.

Naibu waziri huyu alisema kuwa ufugaji wa samaki ni sekta ambayo vijana wanaweza kujitosa ili watumie talanta, ujuzi wao na teknolojia pia.

“Jamii inapoendelea kukua, watu wengi hupendelea kula vyakula vya protini ikilinganishwa na ulaji wao wa nafaka. Kilimo cha samaki ni kati ya bishara zenye pesa nyingi ambayo vijana wanafaa waingilie,” akasema Prof Boga.