Habari

SENSA: Mlipuko wa vijana waja

February 23rd, 2020 2 min read

PETER MBURU na BENSON MATHEKA

MATOKEO ya sensa ya mwaka 2019 yameanika wazi hatari inayokodolea Kenya macho, kutokana na idadi kubwa ya vijana, wengi wao wasio na kazi, ambao pia wanaonekana kuishiwa na matumaini.

Licha ya serikali kuahidi vijana kuwa ingewapa ajira, hali inaonekana kuharibika zaidi hasa kwa kuzingatia takwimu zilizotolewa na Shirika la Takwimu nchini (KNBS).

Takwimu hizo zimeonesha kuwa kati ya Wakenya milioni 47.56 waliohesabiwa Agosti mwaka jana, raia walio na umri wa chini ya miaka 35 ni milioni 35.7, hii ikiwa ni asilimia 75.1 ya Wakenya wote.

“Idadi ya vijana wa kati ya miaka 18 na 34 ilikuwa 13, 777,600 ama asilimia 29 ya jumla ya wananchi waliohesabiwa, ikilinganishwa na watu milioni 11.8 katika sensa ya 2009,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa KMBS, Zachary Mwangi.

Ni vijana wa umri huu ambao kitaifa na kimataifa wanachukuliwa kuwa wenye nguvu na uwezo wa kufanya kazi ipasavyo, na wanafaa kuwa kazini.

Hata hivyo, kati ya idadi hiyo ya vijana, jumla ya 1,647,484 waliohesabiwa (ambao hawako shuleni tena) walisema kuwa hawana na kazi yoyote, licha ya kuwa walikuwa wakitafuta.

Vilevile, kati ya Wakenya milioni 27.2 walio na umri wa kati ya miaka 15 na 64, takriban milioni nane hawakuwa wakifanya kazi yoyote, kwani ni watu milioni 19.7 walioripoti kuwa kazini.

Hii ni licha ya kuwa idadi ya vijana ambao wanazidi kusoma kufikia viwango vya juu imepanda kwa viwango vikubwa, huku kukiwa na zaidi ya wanafunzi 470, 983 katika vyuo vikuu na 506, 109 katika vyuo vya kiufundi na vingine.

Idadi hii imepanda zaidi ikilinganishwa na ya sensa ya 2009, ambapo kulikuwa na wanafunzi 171,855 katika vyuo vikuu na 325,196 katika vyuo vya kiufundi.

“Idadi ya wanafunzi wa shule za msingi ilikuwa milioni 10 na shule za upili milioni 3.4,” akasema Bw Mwangi, akitoa tarakimu zilizoonyesha jinsi Wakenya wanavyozidi kukumbatia elimu.

Lakini licha ya kuzidi kupata masomo ya juu, sekta ya ajira nchini haijakuwawa ikizalisha nafasi nyingi za kazi ili kukidhi mahitaji ya idadi kubwa ya wanaofuzu kila mwaka, mamilioni wakiachwa bila la kufanya.

Hali hii imekuwa ikiathiri taifa, kwani baadhi ya vijana hawa wanaishia wakijihusisha na visa vya uhalifu ili kujipa riziki; kama wizi wa kawaida au kutumia teknolojia. Vijana wanaojihusisha na uhalifu huu wana umri wa miaka 18 na 34.

Vilevile, visa vya maelfu ya vijana waliohitimu vyuoni kuhadaiwa na wakora na kujiunga na makundi ya kigaidi vimekuwa vikiripotiwa; ishara ya tatizo kubwa ambalo ukosefu wa kazi umeleta nchini.

Magenge ya vijana pia yamekuwa yakihangaisha wakazi katika maeneo mbalimbali na idadi ya wanaojitia kitanzi kwa kupoteza matumaini maishani imekuwa ikiongezeka. Wataalamu wamehusisha ongezeko la msongo wa mawazo miongoni mwa vijana na ukosefu wa ajira na hali ngumu ya maisha.

“Vijana wanajumuisha asilimia 75 ya Wakenya wote. Lazima kuwepo mpangilio mzuri wa jinsi tutakavyoshughulikia suala la ukosefu wa kazi miongoni mwao ili kuepuka matatizo baadaye,” Gavana wa Kakamega, Bw Wycliffe Oparanya alisema Jumamosi.

Mwenzake wa Machakos, Dkt Alfred Mutua pia aliunga mkono akisema: “Vijana wamekosa kazi Kenya kwa kuwa kuwekeza Kenya ni vigumu, serikali imefanya mambo kuwa magumu na ndipo vijana wanakosa kazi.”

Takwimu za KNBS, aidha zimeonyesha kuwa idadi ya watu wanaohamia mijini kutoka mashambani imekuwa ikipanda kwa miaka 10 iliyopita, jambo ambalo linaweza kuhusishwa moja kwa moja na wengi kuelimika na kuelekea huko kutafuta kazi. Kwa sasa Wakenya milioni 14.83 wanaishi mijini, kinyume na katika sensa ya 2009 ambapo Wakenya milioni 12.49 ndio waliokuwa mijini.

“Asilimia ya watu wanaoishi mijini ikilinganishwa na Wakenya wote ilipanda kutoka asilimia 24.1 mnamo 2009 hadi asilimia 31.2, 2019,” alisema Bw Mwangi.

Baada ya hali kuharibika zaidi na kuwasakama vijana koo, miezi ya majuzi waliamua kukomesha kimya na kuanza kulalamika kuhusu kutengwa na serikali kwa kunyimwa kazi wakati wazee waliozidi miaka ya kustaafu wakizidi kuajiriwa.