Habari

SENSA: Wakenya 14,000 wana umri wa zaidi ya miaka 100

February 24th, 2020 1 min read

Na PETER MBURU

KENYA ilikuwa na wazee 14,040 wanaozidi umri wa miaka 100 kufikia Agosti 2019, wakati hesabu ya watu kote nchini ilifanywa.

Kulingana na matokeo ya sensa yaliyotolewa na Shirika la Takwimu Nchini (KNBS), asilimia 72.4 ya idadi hiyo ilikuwa wanawake.

Ripoti ya KNBS ilionyesha kuwa hadi wakati wa sensa, kulikuwa na wanaume 3,876 waliokuwa na zaidi ya miaka 100, na wanawake 10,164.

Hata hivyo, hakukuwa na mtu yeyote aliyeripoti kuwa katika sehemu ya watu wa jinsia mbili.

Vilevile, watu ambao hawakuwa wanafahamu umri wao walikuwa 687, kati yao wakiwa wanaume 385, wanawake 297 na watano walioripoti kuwa na jinsia mbili.

Katika sensa ya 2009, idadi hiyo haikurekodiwa, kwani waliohesabiwa walikuwa wa kati ya kuzaliwa hadi miaka 95 pekee.

Sensa hiyo ilirekodi jinsi viwango vya maisha vimepanda miongoni mwa Wakenya kwa mambo ya kimsingi kama mahali pa kuishi, kupata maji safi na kuboreshwa kwa hali ya afya.

Hayo yakiongezwa na hali kuwa serikali imekuwa ikiwapa wazee wa zaidi ya miaka 65 pesa za kiinua mgongo kila mwezi, huenda ndiyo sababu ya kuwepo kwa idadi kubwa ya wazee wakongwe.

Katika ugawaji wa umri kwa makundi, lililoongoza ni la watoto wa kati ya miaka 10 na 14, ambao walikuwa milioni 6.3.

Walifuatwa na wale wa kati ya miaka mitano na tisa waliokuwa milioni 6.2.

Matokeo hayo ya mwaka 2019 pia yalionyesha kuwa idadi ya watoto ambao hawakuwa wametimu mwaka tangu kuzaliwa ilikuwa 105,074, kati yao wakiwa wasichana 552,528, wavulana 552,508 na 38 wa jinsia mbili.