Habari Mseto

SENSA: Walio katika kaunti za mbali waombwa kurejea nyumbani

January 28th, 2019 1 min read

Na Gitonga Marete

VIONGOZI katika Kaunti ya Laikipia wamewaomba wakazi ambao wanafanya kazi katika maeneo ya mbali kurejea nyumbani mnamo Agosti, ili kuhesabiwa kwenye Sensa ya Kitaifa.

Walisema kuwa uwepo wao utaisaidia kuongezwa mgao wa fedha inazopokea kutoka kwa Serikali ya Kitaifa.

Wakiongozwa na Waziri wa Kilimo, Bw Mwangi Kiunjuri, viongozi walisema kwamba kaunti nyingi hazikuandikisha idadi kamili ya wakazi kwani wengi wao hawakuhesabiwa kwenye Sensa ya 2009. Walisema hilo limeathiri pakubwa kiwango cha fedha ambazo zimekuwa zikipokea kutoka Serikali ya Kitaifa.

“Serikali huzingatia idadi ya watu kwenye mchakato wa kuwahesabu. Tutainua kiwango tunachopokea ikiwa tutajitokeza kwa wingi katika makazi yetu ili kuhesabiwa,” akasema Bw Kiunjuri.

Alizungumza hayo mnamo Jumamosi katika kijiji cha Umande, Kaunti Ndogo ya Laikipia Mashariki kwenye mazishi ya Bi Nyawira Mwangi, ambaye alikuwa mfanyabishara mjini Nanyuki.

Kauli yake iliungwa mkono na Seneta John Kinyua na Spika wa Bunge la Kaunti ya Laikipia Patrick Waigwa, aliyesema kwamba eneo hilo lina watu wengi ila wamekuwa wakielekea kwingineko kutafuta ajira.

Mbali na hayo, waliwaomba wazazi kuwashinikiza wanao kurejea nyumbani ili kushiriki katika shughuli hiyo.

Bw Kinyua aliunga mkono matumizi ya mitambo ya BVR kwenye shughuli hiyo, akisema kuwa itasaidia kuimarisha uwazi.

Mbunge Mwanamke Catherine Waruguru alisema kwamba kaunti hiyo inapaswa kuzingatiwa kimaendeleo, kwani imekuwa ikiorodheshwa kama eneo la Mlima Kenya na Bonde la Ufa ila haijakuwa ikinufaika.