Habari

Sensa ya visanga

August 26th, 2019 2 min read

NA WAANDISHI WETU

SHUGHULI ya kuhesabu watu inaingia siku ya tatu Jumatatu kukiwa na ripoti za visa tofauti katika maeneo mengi ya nchi. Katika Kaunti ya Kisumu, mmoja wa maafisa wa kuhesabu watu alibakwa muda mfupi baada ya kufika nyumbani mwendo wa saa saba unusu usiku.

Mkuu wa polisi eneo la Nyanza, Dkt Vincent Makokha, alisema mwanamke huyo alivamiwa na kundi la wanaume waliokuwa na panga, wakambaka kwa zamu kabla ya kutoroka na simu yake, tochi na kifaa cha kuchajia simu.

Hata hivyo, wahuni hao hawakuchukua kifaa cha kurekodi takwimu za watu waliohesabiwa usiku huo wa Jumamosi.

Jamaa wa familia ya msichana huyo aliambia Taifa Leo kwamba baada ya kumnajisi msichana huyo, wahuni hao walimsindikiza hadi nje ya nyumba ya shangazi yake na wakasubiri afunguuliwe mlango kabla ya kutokomea gizani.

Katika kaunti za Homa Bay na Nakuru, maafisa wa kuhesabu watu waliumwa na mbwa. Afisa aliyeumwa Homa Bay alikatiza shughuli na kutafuta tiba hospitalini, baada ya paja lililoumwa kuanza kufura.

Naibu Kamishna wa kaunti ndogo ya Rachuonyo Kusini, Bw Mohamud Ibrahim, alisema afisa huyo alishambuliwa na mbwa wa jirani yake.

“Alikuwa katika eneo anakoishi, akaamua arejee nyumbani usiku kwenda kupata chakula kabla ya kuendelea na shughuli hiyo. Lakini mbwa alimrukia na kumuuma,” akasema Bw Ibrahim.

Katika eneo la Kabati, Naivasha katika Kaunti ya Nakuru, afisa wa kike alishambuliwa na mbwa jana alfajiri na kuumwa mkononi.

Aliambia Taifa Leo kwamba alikuwa ameingia kwenye nyumba moja katika eneo hilo alipokumbana na mbwa mkali aliyeanza kubweka.

“Alijaribu kutoroka lakini mbwa huyo alimfukuza na kumuuma mkono wake wa kulia,” alieleza Naibu Kamishna wa kaunti ndogo ya Naivasha, Bw Mbogo Mathioya.

Katika mtaa wa Nyalenda mjini Kisumu, watu wawili walikamatwa na polisi kwa kukataa kuhesabiwa.

Kamanda wa Polisi wa Kisumu, Bw Benson Maweu, alisema wawili hao, ambao ni mwanamume na mwanamke waliwafukuza maafisa wa sensa wakisema hawakuwa tayari kuhesabiwa.

Katika Kaunti ya Baringo, watu wa jamii ya Ilchamus walikataa kuhesabiwa wakilalamikia hatua ya kuwahesabu kama wakazi wa Baringo Kaskazini badala ya Baringo Kusini.

Wakazi hao walisema juhudi za kutaka suala hilo kurekebishwa lilipuuzwa na kamishna wa Kaunti ya Baringo, Henry Wafula.

Nako Kaunti ya Vihiga, Kamishna Bi Susan Waweru alisema wenye mabaa maeneo ya Chavakali na Shamakhokho watachukuliwa hatua kwa kukaidi agizo la kufunga biashara zao.

“Nitakuwa na mazungumzo na wamiliki wa baa hizo. Inasikitisha kuwa mmoja wa machifu wangu alionekana kwenye mojawapo ya baa hizo na nimeagiza akamatwe,” akasema Bi Waweru.

Katika kaunti ya Tana River, polisi walisimamisha harusi ya mwana wa mwanasiasa mashuhuri wakisema ilihitilafiana na saa za shughuli za kuwahesabu watu.

Hashim Daud, mwanawe Mbunge Mwakilishi wa Wanawake Tana River, Bi Rehema Hassan, alitarajiwa kumvisha pete Aisha Jineri, bintiye Mkurugenzi wa elimu za Chekechea, Johora Hassan.

Kulingana na tamaduni za Kiislamu, baadhi ya harusi hufanywa usiku, ambapo watu hukusanyika kwa karamu.

Jijini Nairobi waraibu wa pombe katika mitaa ikiwemo Githurai, Umoja, Nairobi West na Kangemi walifungiwa ndani ya mabaa kuendelea kulewa kinyume na amri ya Waziri wa Usalama wa Nchi, Fred Matiang’i kuwa zifungwe saa kumi na moja jioni.

Televisheni zilizimwa sauti na wakawa wanazungumza kwa sauti za chini ili wasijulikane walikuwa ndani.

Ripoti za Rushdie Oudia, Stephen Oduor, George Odiwuor, Derrick Luvega na Macharia Mwangi