Habari

Sensa yaanza kote nchini maafisa wakiambiwa kulinda vifaa

August 24th, 2019 1 min read

Na WAANDISHI WETU

SHUGHULI ya kuhesabu watu imeanza Jumamosi saa kumi na mbili jioni ilivyopangwa huku maafisa wanaoitekeleza wakionywa dhidi ya kupoteza vifaa vya kidijitali wanavyotumia.

Rais Uhuru Kenyatta na familia yake wanahesabiwa Jumamosi saa nne usiku; shughuli itakayoendeshwa na katibu wa Wizara ya Mipango Julius Muia pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS) katika Ikulu ya Nairobi.

Msemaji wa Serikali Kanali (Mstaafu) Cyrus Oguna amekariri umuhimu wa shughuli hiyo akisema itasaidia serikali katika mipango yake ya kuhudumia wananchi.

“Shughuli hii ni muhimu kwani itaiwezesha serikali kufanya mipango kwa mtoto wako ambaye atazaliwa na wale ambao hawajazaliwa,” amesema.

Bw Oguna amesema kuwa kwa mara ya kwanza data zitakusanywa kwa kutumia mitambo ya kielektroniki ambayo itahifadhi maelezo yote kuhusu Wakenya kwa njia salama.

“Hitaji kwamba utoe kitambulisho cha kitaifa au paspoti hailengi kuchunguza mienendo yako bali ni njia ya kujua idadi ya Wakenya ambao wametimu umri wa kupata stakabadhi hizo lakini hawana. Tusikosoe shughuli hii. Maafisa wa kuhesabu wakibisha mlango wako tafadhali fungua,” akahimiza. Alikuwa ameandamana na Mkurugenzi Mkuu wa KNBS Zachary Mwangi.

Chonjo

Kuhusu usalama, Kanali Oguna amethibitisha kuwa maafisa wa usalama wa kutosha wamewekwa chonjo kudumisha amani ndani ya kipindi chote cha sensa, kuanzia Agosti 24 hadi Agosti 25.

Amewashauri wananchi kujulisha maafisa wa usalama kuhusu visa vyovyote vya utovu wa usalama kwa kupiga simu nambari 0800221020 ambayo haitatozwa ada yoyote.

Kanali Oguna ameongeza kuwa serikali imewakodi wataalamu wa lugha za ishara kuwasaidia watu ambao ni viziwi kushiriki sensa.

“Hata hivyo, mikakati mingine imewekwa kuhakikisha kuwa watu wenye aina nyingine ya ulemavu, kama vile wenye akili punguani, wanasaidiwa,” ameongeza.

Wakati huo huo vifaa vya kuhesabu watu viliibwa katika kituo cha Siyoi, Kaunti ya Pokot Magharibi mnamo Alhamisi usiku.