Makala

Sera duni kuhusu ajira, SMEs ndicho kiini cha ufukara Kenya – utafiti

January 29th, 2020 2 min read

Na MARY WANGARI

SERA duni zinazowabagua wamiliki biashara ndogondogo na za wastani (SMEs) pamoja na ajira isiyo rasmi ndicho kiini cha ufukara nchini Kenya, utafiti mpya umeibua.

Kulingana na ripoti mpya ya Benki ya Dunia kuhusu Michakato ya Thamani kuhusu uzalishaji, ukosefu wa ajira rasmi ndicho chanzo cha ufukara na kudhoofika kiuchumi miongoni mwa waajiriwa katika sekta ya kilimo nchini.

Aidha, uchunguzi huo uliohusisha tafiti 49 kuhusu uzalishaji bidhaa ulidhihirisha kwamba “ukosefu wa urasmi ndio ukawaida badala ya kuwa suala la kipekee: Idadi kubwa ya wafanyakazi hawana kandarasi rasmi hata katika kampuni rasmi.”

Utafiti huo ulijumuisha data iliyokusanywa kutoka kwa wakulima 1,200 kutoka Kenya, Ghana na Zambia wanaokuza nafaka na ulidhihirisha kwamba Kenya inaongoza barani Afrika kwa idadi ya waajiriwa wasio na kandarasi ikifuatiwa na Zambia.

“Asilimia 97 ya wafanyakazi katika sekta ya kilimo nchini hawana kandarasi ikifuatiwa na Zambia kwa asilimia 82. Hata kwa waajiriwa walio na kandarasi, asilimia 86 wana kandarasi zisizo rasmi,” ilisema ripoti hiyo iliyotiwa sahihi na rais wa Benki ya Dunia David R. Malpass.

Ripoti hiyo pia ilieleza umuhimu wa kuimarisha SMEs ambazo zinajumuisha asilimia kubwa ya mapato ya maskini, kupitia ufadhili wa huduma za kilimo, vifaa vya kukabiliana na majanga pamoja na usimamizi mwafaka ili kunufaika kutokana na viwanda vikuu vya uzalishaji.

“Asilimia 55 ya kazi barani Afrika zimo katika sekta ya kilimo ambayo inajumuisha asilimia 70 ya mapato ya maskini. Thamani ya kilimo katika mataifa huathiriwa na mbinu za kijadi zisizo rasmi zinazowaathiri kihasi wafanyakazi kupitia ufukara na kukosa kujiimarisha kifedha,”

“Ili kudhibiti viwango vya ufukara nchini na kuimarika kiuchumi ni sharti Kenya ibuni sera maalum zitakazowezesha kuunganisha SMEs na viwanda vikuu nchini humo,”

Kando na hayo, ripoti hiyo imehimiza Kenya na mataifa mengine yanayoegemea kilimo barani Afrika kubuni sera zitakazounganisha SMEs na mashirika makubwa nchini mwao kupitia kufadhili mafunzo, uhamasishaji pamoja na kutoa habari kwa mashirika makuu kuhusu nafasi za usambazaji bidhaa.

Japo wakulima wanaomiliki mashamba madogomadogo pamoja na vibarua ni sehemu ya nguzo za uzalishaji, ukosefu wa usawa unaathiri uzalishaji nchini na kulemaza ukuaji wa uchumi.