Sera ya wajawazito kuingia darasani ifutwe, walimu warai

Sera ya wajawazito kuingia darasani ifutwe, walimu warai

Na CHARLES WANYORO

WALIMU wa shule za upili katika eneobunge la Tigania Magharibi, wameitaka serikali kubatilisha sera yake ya kutaka wanafunzi wa kike waliopata uja uzito kusalia shuleni.

Walisema sera hiyo itachangia ongezeko la visa vya wanafunzi wa kike kupata uja uzito wakiwa shuleni.

Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Upili (KESSHA) katika kaunti hiyo ndogo Martha Githinji alisema wameshindwa kulaani visa hivyo kwa sababu wamelazimishwa kuwadumisha shuleni wanafunzi waliopata uja uzito.

Alisema wenzake hawako tayari kuwa na wanafunzi wenye uja uzito na wanaonyonyesha na wakaitaka Wizara ya Elimu kubatilisha sera hiyo kama njia ya kupalilia maadili miongoni mwa wanafunzi wa kike.

Akiongea katika soko la Kianjai ambapo walimu wakuu wa shule 50 za upili na wengine 135 wa shule za msingi walipokea matangi ya maji kutoka kwa kamati ya CDF, Bi Githinji alipendekeza kuwa wasichana wenye uja uzito wanapaswa kukaa nyumbani.Matangi hayo ya lita 3,000 yanalenga kusaidia katika mpango wa utekaji wa maji.

“Tunaomba serikali iangalie upya sera hiyo… Wanafunzi kama hao wanaweza kusalia nyumba hadi watakapojifungua. Baada ya hapo wanaweza kurejea shuleni na kwa namna hii tudumishe nidhamu katika jamii. Tusiporekebisha hili, wanafunzi wengine wa kike wataiga mwenendo huo au wao wao wakarudia uovu huo,” Bi Githinji akasema.

Kaunti ya Meru ni miongoni mwa zile ambazo ziliandikisha idadi kubwa ya watahiniwa wa kike wa mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE) waliofanya mtihani huo wakiwa na uja uzito.

Bi Githinji, ambaye ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Mituntu, alisema wenzake wameshindwa kuwashauri wanafunzi wa kike dhidi ya kupata mimba za mapema.Hii ni kwa sababu wanawaona wenzao ambao wana uja uzito wakiendelea na masomo kama kawaida.

Bi Githinji alisema inaonekana kuwa serikali imeshindwa kushughulikia kero za mimba za mapema shule. Kwa hivyo, alitoa wito kwa wazazi na wanajamii kwa ujumla kuwafunza matineja kuhusu hatari na madhara ya mimba za mapema.

“Wanafunzi hawa huwa hawapachikwi mimba shuleni bali nje ya shule. Tunapolazimishwa kuwadumisha shuleni wanafunzi wenye mimba hadi watakapojifungua, tutashindwa kabisa kuwashauri wenzao kwamba ni makosa kupata uja uzito kabla ya kukamilisha masomo,” akasema Bi Githinji.

You can share this post!

BENSON MATHEKA: Serikali haifai kupuuza ripoti ya Human...

Wazimamoto wafaidika kwa mafunzo ya kisasa