Serena abanduliwa Canadian Open

Serena abanduliwa Canadian Open

NA MASHIRIKA

TORONTO, Canada

SUPASTAA Serena Williams amekiri kuwa yeye si mzuri katika kupeana kwaheri baada ya Mwamerika huyo kupoteza mchuano wa kwanza tangu adokeze anapanga kustaafu kutoka tenisi.

Serena alipepetwa 6-2, 6-4 katika raundi ya pili na Belinda Bencic kwenye shindano la National Bank Canadian Open, jana Alhamisi.

Hiyo ni siku moja baada ya mshindi huyo wa mataji 23 ya Grand Slam kufichua kupitia jarida la Vogue kuwa “ameanza kujiandaa kwa maisha baada ya tenisi” na anapanga kustaafu tenisi ambayo ametawala kwa miaka 20.

“Bila shaka kilikuwa kitu kinacholeta hisia nyingi,” Serena aliambia mashabiki mnamo Alhamisi.

“Napenda kucheza hapa, kila mara nimefurahia kucheza hapa. Natamani ningecheza vyema, lakini Belinda alicheza vizuri sana leo. Zimekuwa saa 24 za kutia moyo.

“Nilivyoandika katika jarida hilo, mimi si mzuri katika kusema kwaheri. Hata hivyo, kwaheri Toronto,” alisema Serena akifuta machozi na kuwashukuru mashabiki waliompa shukrani pia baada ya nyota huyo kupokea zawadi kutoka kwa timu ya mpira wa magongo ya Toronto Maple Leafs na mpira wa vikapu ya Toronto Raptors.

  • Tags

You can share this post!

DOMO: Kagundua followers sio wapigakura

Wakenya kusubiri zaidi kabla kumjua rais mpya

T L