Serge Aurier ajiunga na Villarreal ya Uhispania

Serge Aurier ajiunga na Villarreal ya Uhispania

Na MASHIRIKA

BEKI wa zamani wa Tottenham Hotspur, Serge Aurier, amejiunga na kikosi cha Villarreal kinachoshiriki Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Beki huyo raia wa Ivory Coast mwenye umri wa miaka 28, alikuwa mchezaji huru baada ya mkataba wake na Spurs kutamatika mwishoni mwa Agosti 2021.

Chini ya kocha Unai Emery, Villarreal ambao ni washikilizi wa taji la Europa League, watakuwa huru kurefusha kandarasi ya Aurier kwa miaka miwili zaidi mwishoni mwa msimu huu wa 2021-22. Hivyo, upo uwezekano mkubwa kwamba beki huyo wa kulia atuhudumu kambini mwa Villarreal hadi mwaka wa 2024.

Aurier alichezea Spurs kwa kipindi cha miaka minne baada ya kusajiliwa kutoka Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa kwa Sh3.6 bilioni mnamo Agosti 2017.

Kufikia sasa, Villarreal wanashikilia nafasi ya 11 kwenye msimamo wa jedwali la La Liga baada ya kujizolea alama 11 kutokana na mechi saba za ufunguzi wa kampeni za muhula huu. Japo walijituma vilivyo dhidi ya Manchester United kwenye gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Septemba 29, 2021, walipokezwa kichapo cha 2-1 katika mchuano huo wa mkondo wa kwanza uwanjani Old Trafford.

Aurier ataingia kambini mwa waajiri wake wapya baada ya kukamilika kwa mechi mbili zijazo za kimataifa zitakazokutanisha Ivory Coast na Malawi nyumbani na ugenini.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

NASAHA: Fanya uamuzi wa dhati kuhusu taaluma uitakayo...

KAULI YA MATUNDURA: Ken Walibora anavyoendeleza taswira ya...