HabariSiasa

Serikali haikupewa agizo na korti yoyote, Miguna hakufurushwa – Matiang'i

April 3rd, 2018 1 min read

JOHN NGIRACHU na ELVIS ONDIEKI

WAZIRI wa Usalama Dkt Fred Matiang’i Jumanne ametetea vikali serikali kuhusu jinsi ilishughulikia kesi ya wakili mbishi Dkt Miguna Miguna na alivyohangaishwa katika uwanja wa JKIA alipotua kutoka Canada,.

Akihojiwa pamoja na Mkuu wa Polisi Joseph Boinnet na Kamati ya Bunge kuhusu Usalama katika jumba la Continental, waziri huyo alitumia fursa hiyo kuitetea wizara yake dhidi ya kumzuia kuingia nchini, kumtesa, na kumfurusha hadi Dubai raia mzaliwa wa Kenya na mwenye kitambulisho halisi.

Wakuu hao wa serikali juma lililopita walikaidi agizo la kufika mahakamani kuelezea sababu za kufurushwa kwa Miguna, hali iliyopelekea korti kuwapata na hatia na kuwapiga faini ya Sh200,000 kila mmoja.

Lakini Jumanne, Dkt Matiang’i alisema waziwazi kuwa serikali haikupewa agizo lolote na korti yoyote, huku akikanusha kuwa Dkt Miguna alizuiwa kuingia nchini kinyume cha sheria.

“Wakili Miguna aliondolewa tu kutoka eneo la JKIA, na wala hakufurushwa, kwa kuwa wakati huo hakuwa nchini Kenya,” aliambia wabunge.

Waziri huyo alijitetea kuwa mawakili na jamii ya kutetea haki za binadamu walilenga kuiaibisha na kuitishia serikali kwa kuwa yeye hakupokea agizo lolote kati ya maagizo matatu yaliyotolewa na korti.

Alikariri kuwa mahakama ilikuwa inatumiwa kuhujumu mamlaka ya serikali, huku akiepuka kutaja jaji au wakili yeyote kwa jina.

Kuhusu hatima ya Dkt Miguna ambaye alisafiri Canada Jumatatu, waziri huyo alisema kuwa “Miguna yuko huru kujisajili rasmi kupewa uraia wa Kenya na kurudi nchini wakati wowote atakao.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji Gordon Kihalangwa alikana kuwa Dkt Miguna alizuiliwa kwa choo katika uwanja wa JKIA, akisema kuwa “Miguna alikuwa kwa chumba chenye godoro na choo.”