Serikali haitaweka vikwazo dhidi ya wageni kuingia Kenya kufuatia mlipuko wa aina mpya ya corona

Serikali haitaweka vikwazo dhidi ya wageni kuingia Kenya kufuatia mlipuko wa aina mpya ya corona

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI ya Kenya haina mipango ya kuwazuia wasafiri kutoka mataifa yaliyoathirika na aina mpya ya virusi vya Covid-19 aina ya Omicron.

Akiongea na wanahabari Jumapili katika kaunti ya Kisii, Katibu katika Wizara ya Afya Susan Mochache alisema serikali inaendesha ukaguzi katika maeneo yote ya mipaka ambapo watu wote wanakaguliwa kubaini ikiwa wamepata chanjo.

“Japo imethibitishwa kwamba aina mpya ya virusi vya Covid-19 vimegunduliwa nchini Afrika Kusini, serikali haina mipango ya kuzuia watu kutoka taifa hilo na mataifa mengine jirani kuingia Kenya. Kile serikali inafanya ni kuhakikisha kuwa kila mgeni anayeingia kupitia maeneo ya mipaka amepata chanjo,” Bi Mochache akasema.

Katibu huyo aliwahimiza Wakenya kuendelea kujitokeza kupata chanjo na wazingatia masharti yaliyowekwa na serikali ya kuzuia msambao wa corona.”Wakenya waendelea kupokea chanjo. Na visa vya maambukizi vikiendelea kuwa chini kiasi hiki, serikali itaendelea kuruhusu watu kuendelea na shughuli zao za kiuchumi kama kawaida.

“Tunatarajia kuwaruhusu Wakenya kuendelea na shughuli za kibiashara haswa wakati wa msimu huu wa sherehe wakati ambapo sekta ya utalii inatarajiwa kuimarika,” Bi Mochache akaongeza Katibu huyo aliwahimiza wananchi kuendelea kuvalia barakoa, kudumisha usafi na kutosongamana katika mikutano mikubwa ili kuzuia visa vya maambukizi mapya ya Covid-19.

Aina ya virusi ya Omicron ilichipuza nchini Afrika Kusini mapema mwezi huu wa Novemba kabla ya kusambaa katika mataifa jirani ya kusini mwa Afrika kama vile Namibia, Botswana na Eswati.

Wanasayansi wanasema aina hiyo ya virusi inasambaa kwa kasi kuliko virusi aina ya Delta iliyogunduliwa nchini India mwanzoni mwa mwaka huu.

You can share this post!

Aliyetekwa arudi nyumbani baada ya miezi mitano

Sh20m kutumiwa kukarabati jengo la makavazi

T L