Habari Mseto

Serikali ibadilishe mbinu inayotumia kukabiliana na wizi wa mifugo – wabunge 

January 29th, 2024 2 min read

NA OSCAR KAKAI

JUHUDI za kutafuta amani eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa zimepata pigo majangili wakishambulia na kuua askari wa akiba (NPR). 

Shambulizi hilo limelazimisha baadhi ya wabunge kuitaka serikali kubadilisha mbinu yake inavyokabiliana na wizi wa mifugo maeneo yaliyoathirika Kerio Valley.

Afisa huyo wa NPR aliuawa mnamo Ijumaa, Januari 26, 2024.

Mashambulizi hayo yamefanyika majuma mawili baada ya Wizara ya Usalama wa Ndani kutuma askari 205 wa akiba Pokot Magharibi kulinda maeneo hatari ya mipaka kama Turkwel na  Chesegon.

Hali ya taharuki inaendelea kutanda katika maeneo hayo baada ya washukiwa wahuni kuvamia kijiji cha Chepkoiket, eneo la Takaywa, Kaunti Ndogo ya Pokot Kaskazini na kuua Lotuliamuk Lokomol ambaye alikuwa anashika doria katika shule ya msingi ya Lonyangalem.

Akithibitisha tukio hilo, Chifu wa Ombolion Joseph Korkimul alisema wakazi wanaishi kwa hofu akidokeza kwamba maafisa wa usalama bado wanasaka wakora ambao wanaaminika kutoka eneo la Kaptir, Kaunti jirani ya Turkana.

Bw Korkimul pia alithibitisha kuwa Alhamisi, Januari 25, 2024, majangili kutoka eneo la  Kaptir walijaribu kuiba idadi isiyojulikana ya mifugo lakini maafisa wa usalama walitibua njama zao.

Kulingana na Bw Korkimul, Wizara ya Usalama wa Ndani inafaa kuongeza askari wa akiba katika eneo hilo ili kusaidia kupambana na wezi wa mifugo na kutuliza hali katika eneo hilo.

Viongozi kutoka Kaskazini mwa Bonde la Ufa , wameshutumu shambulio la hivi punde.

Wakizungumza katika maziko ya Pasta Mary Moroto, mkewe Mbunge wa  Kapenguria Dkt Samuel Moroto ambaye aliaga dunia kutokana na ugonjwa wa Saratani, walishutumu mauaji hayo wakiitaka serikali kubadilisha mbinu ambazo inatumia kukabiliana na majangili.

“Mtu alipigwa risasi na kujeruhiwa vibaya leo. Kama wabunge lazima tufanye tunachosema, kwa kuhamasisha umuhimu wa amani,” alisema Seneta wa Kaunti ya Pokot Magharibi, Julius Murgor.

Gavana wa Pokot Magharibi, Simon Kachapin alisema kuwa eneo hilo ni tulivu japo alitaja majangili wachache ambao wanavuruga amani.

“Siku zao zimefika. Ni wahuni wachache tu wanatuhangaisha. Tunawashutumu na tusilaumiane. Jamii tunazopakana nazo, sote hufanya biashara pamoja ,” alisema Gavana Kachapin.

Naye mwenzake wa Elgeyo Marakwet Wesley Korir alisema ni aibu kizazi cha sasa kupoteza katika mashambulizi na kuiba mifugo.

“Sisi kama magavana wa kaunti zinazoshuhudia wizi wa mifugo na mashambulio ya mara kwa mara, tumeapa lazima tukomeshe suala hili,” Bw Korir akaahidi.

Wabunge wengine waliohudhuria mazishi ya mkewe wa Samuel Moroto ni Ndindi Nyoro (Kiharu), wa Turkana Kusini, John Ariko, na mbunge maalum Jackson Kosgei, wote wakihimiza haja ya kudumisha amani Kerio Valley.