Serikali ichunguze ‘shule bandia’ zinazodaiwa kuwafundisha wageni lugha

Serikali ichunguze ‘shule bandia’ zinazodaiwa kuwafundisha wageni lugha

KATIKA kipindi cha miezi kadhaa sasa, kumezuka madai kuwa kuna shule ambazo hazijasajiliwa katika kaunti ya Nairobi zinazowafunza wageni lugha ya Kiswahili ili baadaye waweze kuitumia kwa manufaa yao wenyewe.

Kuna tetesi kwamba wengi wa wageni hawa, baada ya kufunzwa Kiswahili hudai kuwa ni Wakenya hivyo basi kutaka kujisajili kama raia wa taifa la Kenya.

Mafunzo hayo yanaendelea katika makazi ya watu binafsi, na baadhi ya shule zinazojiita za Shule za Kimataifa.

Wizara ya Elimu inafaa kufuatilia madai haya na kukagua sehemu zinazotumika kuendesha mafunzo hayo.

Itakuwa muhimu kubaini silabasi inayotumika na pia uhitimu wa walimu wanaoendesha mafunzo hayo.

Serikali inafaa kukaa macho na idara inayohusika na kutoa vitambulisho vya taifa kuziba mianya ya aina yoyote ambayo huenda ikapatia watu nafasi ya kusajiliwa kwa mlango wa nyuma.

Vile vile, wizara ya elimu ilinde elimu na matumizi ya lugha yetu ya taifa kwa kuhakikisha kuwa shule ambazo hazizingatii utaratibu kamili kama inavyopendekezwa na serikali, zinafungwa.

Itakuwa hasara kubwa kwetu kama nchi kuruhusu watu ambao hawajahitimu kama walimu kufunza shuleni hasa mambo ambayo hayapo katika utaratibu au mtaala wa elimu.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Kenya itangaze msimamo thabiti kuhusu mashoga

TAHARIRI: Serikali idhibiti mashirika yanayopeleka Wakenya...

T L