Habari MsetoSiasa

Serikali ielezee Wakenya kuhusu BBI kwa kina – Wanaharakati

December 5th, 2019 1 min read

Na GERALD BWISA

WANAHARAKATI wa haki za binadamu katika Kaunti ya Trans Nzoia wanaitaka Serikali kuanza mpango wa kutoa mafunzo kwa Wakenya kuhusu ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI).

Mshirikishi Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Watu Walemavu (IDPN) Bw Raphael Eyanai alisema kwamba mafunzo hayo yatahakikisha kuwa Wakenya wanaelewa mapendekezo hayo kwa kina.

“Mafunzo hayo yatahakikisha kuwa wale ambao hawana uwezo wa kusoma, kuandika ama kuelewa lugha iliyotumika wameielewa ripoti hiyo. Hilo litawawezesha kufanya maamuzi muhimu kuihusu,” akasema Bw Eyanai.

Akihutubu mjini Kitale, mshirikishi huyo alisema kuwa ikiwa Wakenya hawatapewa mafunzo kuhusu ripoti hiyo, huenda wakapotoshwa na wanasiasa.

Alisema kuwa huenda hilo likaathiri maamuzi yao ikiwa kutakuwa na kura ya maamuzi.Alisema kuwa mafunzo hayo yanapaswa kuendeshwa kuanzia kiwango cha wadi kwa kuyashirikisha mashirika ya kidini na yale ya kutetea haki za binadamu ili kuhakikisha kuwa wananchi wengi zaidi wamefikiwa.

Kwingineko, mbunge wa kwanza Bw Ferdinard Wanyonyi amejiunga na viongozi wanaoshinikiza ripoti hiyo kujadiliwa na kupitishwa na Bunge la Kitaifa.

“Kuandaa kura ya maamuzi kutatugharimu pesa nyingi. Kando na hayo, kunaweza kuigawanya zaidi kwa misingi ya kikabila na kisiasa, hasa tunapokaribia uchaguzi mkuu wa 2022,” akasema Bw Wanyonyi.

Mbunge huyo alimwambia Spika wa Bunge Bw Justin Muturi kukoma kutoa kauli kuhusu ripoti hiyo hadharani kuhusu mwelekeo ambao itachukua.

Alisema kuwa hapaswi kuegemea upande wowote kutokana na nafasi anayoshikilia.Baadhi ya vijana katika eneo hilo wameeleza tashwishi yao kuihusu, wakisema kuwa huenda baadhi ya mapendekezo yake kuhusu njia za kuwainua kiuchumi yakakosa kutekelezeka.