Serikali ifadhili elimu ya juu ya madaktari – CoG

Serikali ifadhili elimu ya juu ya madaktari – CoG

Na WINNIE ATIENO

MAGAVANA sasa wanataka Serikali Kuu iwalipe madaktari wanaotaka kujiongeza masomo, wakisema hawana bajeti ya kufadhili mpango huo.

Akiongea jijini Mombasa jana Alhamisi, mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Martin Wambora alisema kuwa serikali za kaunti zitawasilisha kwa Wizara ya Afya na ile ya Fedha takwimu za madaktari wanaoamua kujisajili kwa masomo ya juu.

“Wizara ya Afya sharti ilipe madaktari wanaotaka kujiongeza masomo kwa sababu hatuna bajeti ya mpango huo. Kuanzia sasa mafunzo hayo sharti yalipiwe na Wizara ya Afya wala sio serikali za kaunti,” Bw Wambora akasema katika mkutano wa mashauriano katika hoteli moja mjini Mombasa.

Bw Wambora ambaye ni Gavana wa Embu alisema kila mwaka serikali za kaunti zitawasilisha kwa Wizara za Afya na Fedha orodha ya madaktari waliojisajili kwa masomo ya uzamili “ili mpango huo utengewe fedha.”

Akiunga mkono kauli hiyo, mwenyekiti wa kamati ya CoG kuhusu Afya, Profesa Anyang’ Nyong’o, alisema chini ya Katiba ya sasa, Serikali ya Kitaifa inasimamia masuala ya sera, mafunzo na viwango vya ubora.

“Tutakuwa tunajidunga mwiba miguuni ikiwa hatutatoa mafunzo kwa wafanyakazi wetu. Ili mtu awe muuguzi au daktari shupavu, sharti apate mafunzo tosha. Tumejitolea kwa mafunzo hayo ila hatuna fedha za kugharamia mpango huo,” akasema.

Gavana huyo wa Kaunti ya Kisumu, akaongeza: “Tunataka serikali ya kitaifa itekeleze wajibu wake wa kusimamia masuala ya sera na mafunzo, nasi tutekeleze wajibu wa utoaji wa huduma za afya.”

Prof Nyong’o alisema serikali za kaunti pia zina taasisi za mafunzo kama vile hospitali za rufaa ambako wahudumu wa afya hupokea mafunzo wakiwa kazini.

Mbunge wa Seme, Dkt James Nyikali, alipongeza mpango wa mafunzo ya ziada kwa wahudumu wa afya akisema utapiga jeki mpango wa utoaji huduma za afya.

“Wakati wa mafunzo ya ziada kwa madaktari, huwa hawaketi tu madarasani bali wao huendelea kufanyakazi. Ikiwa madaktari wanafunzwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), wangali wafanyakazi wao. Wakiondolewa, shughuli za KNH zitatatizika mno,” akasema Dkt Nyikal aliyewahi kuhudumu kama Katibu katika Wizara ya Afya na pia Mkurugenzi wa Afya Nchini.

Akaongeza, “Kwa hivyo, ni muhimu kwa wizara ya afya kuwalipa madaktari hao wakifanya kazi huko.”

You can share this post!

Huzuni naibu wa chifu akidaiwa kuuawa na mkewe

Njuki tayari kuingia kambi ya Ruto lakini kwa masharti

T L