Kimataifa

Serikali ikate fungu la kumi kwenye mishahara ya waumini – Askofu

October 31st, 2018 1 min read

DAILY MONITOR Na PETER MBURU

MHUBIRI mmoja kutoka Kampala, Uganda ametoa pendekezo lisilo la kawaida, kuwa serikali iwe ikiwakata waumini fungu la kumi kwenye mshahara na kutuma pesa hizo katika makanisa.

Askofu Mkuu huyo wa kanisa katoliki alisema kuwa Wakristo wengi hawajakuwa wakitoa sadaka, jambo ambalo limeathiri miradi ya kanisa.

“Kila tunapoitisha sadaka, watu wanatoa tu kile walicho nacho kwa wakati huo, lakini Biblia inasema kuwa asilimia kumi ya kile unachopata kiende kanisani,” akasema Mhubiri Lwanga katika kanisa la St Mary’s Cathedral Rubaga wakati wa misa.

“Niungeni mkono ninapotoa pendekezo hili kwa kuwa ni njema kwetu. Hamchoki kutia pesa vikapuni kila wakati?”

Mhubiri huyo alisema kuwa anataka Uganda kuchukua mkondo wa Ujerumani ambapo fungu la kumi kwa waumini wa katoliki hukatwa kwenye mshahara kila baada yam waka.

Ushuru huo wa kanisa hukusanywa na serikali na baadaye kuelekezwa kwa makanisa tofauti.

“Niliambiwa kuwa Wajerumani hufanya makubaliano na serikali ikate fungu la kumi kila mwezi kisha kuzipa kanisa na pesa hizo hutumiwa kujenga makanisa,” akasema.

Wale wasiotaka kulipa fungu la kumi nchi hiyo huandika barua rasmi wakisema kuwa wameamua kuwacha kanisa kwa sababu ya hali hiyo na mara mtu anapoondoka hawezi kula sakramenti tena ama kufanya shughuli za kanisa.