Serikali ilipe bili za wagonjwa wanaofariki wakitibiwa – Jicho Pevu

Serikali ilipe bili za wagonjwa wanaofariki wakitibiwa – Jicho Pevu

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wameitaka serikali kuu kufutilia bili za hospitali za wagonjwa ambao hufariki wakipokea matibabu katika hospitali za umma za rufaa.

Wakiunga mkono hoja iliyowasilishwa na Mbunge wa Nyali Mohammed Ali almaarufu ‘Jicho Pevu’, wabunge wa mirengo ya serikali na upinzani walisema ni kinyume cha Katiba kwa hospitali kukataa kuachilia maiti ya Wakenya masikini.

“Ni unyama na kinyume cha Katiba kwa hospitali kukataa kuachilia maiti ilhali Wakenya wengi ni masikini na hawawezi kumudu gharama ya kulipa ada za hospitali,” Mbunge Mwakilishi wa Nairobi Esther Passaris akasema.

Akianzisha mjadala kuhusu hoja hiyo, Bw Ali alisema kuwa kulingana na Ibara ya 43 ya Katiba, ni haki ya kila Mkenya kupata huduma za matibabu, inayojumuisha haki ya kupata huduma za kimatibabu kwa wagonjwa wote.

“Hata hivyo, ni kinaya kwamba huduma hizo zimekuwa ghali katika hospitali za umma na zile za kibinafsi kiasi kwamba Wakenya wengi hawawezi kupata haki hii ya kikatiba,” akasema Bw Ali.

Mbunge huyo pia aliitaka serikali kudhibiti ada ya mochari katika hospitali za umma akisema ada zinazotozwa wananchi wakati huu ni juu mno.

Mbunge huyo pia anataka kubuniwe kwa Tume maalum ya kusimamia sekta ya afya nchini ili kulainisha shughuli katika sekta hiyo.

Mwaka jana, Mbunge wa Nyando Jared Okello aliwasilisha pendekezo sawa na lake Bw Ali alipopendekeza marekebisho yafanyiwe mswada wa Afya ili kuadhibu hospitali ambazo hukataa kuachilia wagonjwa au maiti kwa sababu ya kutokamilishwa kwa ada.

Bw Okello aliibua wazo hilo kupitia marekebisho aliyowasilisha kwa Mswada wa marekebisho wa Sheria za Afya wa mwaka wa 2018.

You can share this post!

Aapa kwa jina la Mola mara 7 akidai polisi walimuumiza...

Dhuluma za kimapenzi dhidi ya watoto zikomeshwe –...

adminleo