Habari za Kitaifa

Serikali ilivyosukuma Kuppet kufuta mgomo wa walimu


IMEFICHUKA kuwa Tume ya Huduma za Walimu (TSC) ilitumia mbinu za ushawishi, vitisho na kuinyima fedha kukilazimisha Chama cha Kutetea Masilahi ya Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Kadri (Kuppet) kufutilia mbali mgomo wao Jumatatu jioni.

Aidha, baadhi ya wanachama wa Bodi ya Kuu ya Kitaifa (NEB) ya chama hicho pia wamedaiwa kuwa ndumakuwili na kuendeleza masilahi ya serikali sambamba na yale ya Kuppet.

Mnamo Jumatatu, Septemba 2, 2024, maafisa wa Kuppet walipokuwa wakiingia katika makao makuu ya TSC kwa mkutano na maafisa wa tume hiyo, ilikuwa imewanyima makato ya wanachama ya mwezi Agosti.

Tume hiyo ilikataa kukata pesa hizo na kuziwalishwa kwa Kuppet, ilhali huu ni wajibu wa TSC kulingana na makubaliano kati ya asasi hizo mbili.

Ni mbinu kama hii ambayo TSC ilitumia kuilemaza kifedha Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut) mnamo 2019 nyakati ambapo Wilson Sossion alihudumu kama Katibu Mkuu.

Hatua ya TSC kutowasilisha makato ya kila mwezi kutoka kwa wanachama wa Kuppet kutaathiri pakubwa uwezo wa chama hicho kuendesha shughuli zake sawasawa.

Bila fedha Kuppet itashindwa kulipa mishahara ya maafisa wake wa kitaifa na wale wa matawi yake na kuweza kuendeleza mgomo.

Ikiwa na wanachama 135,000, Kuppet hupokea Sh35 milioni kila mwezi kutokana na makato kutoka kwa mishahara ya wanachama.

Kila mwanachama huchangia asilimia 1.8 ya mishahara yao kwa Kuppet kila mwezi.

Pesa hizo hutumika kugharamia shughuli za kila siku katika makao makuu na afisi za matawi, mishahara, ada za mawakili miongoni mwa shughuli zingine.

“Ikiwa TSC imedinda kuwasilisha makato ya kila mwezi, wanachama wetu watahitajika kutafuta njia mbadala za kuifadhiliwa Kuppet ili iendelee kuwa thabiti,” Katibu Mkuu Akello Misori akasema kabla ya kukubaliana na matakwa ya TSC.

Kuppet pia ilikabiliwa na tishio la kuondolewa kutoka orodha ya vyama vya kutetea masilahi ya wafanyakazi vinavyotambuliwa na Wizara ya Leba na vyenye kibali cha kukusanya michango ya kila mwezi kutoka kwa wanachama.

Tishio hilo, ambalo pia liliekezwa Knut mnamo 2021, lilichochea uamuzi wa wanachama wa Bodi Kuu ya Kitaifa (NEB) ya Kuppet kufutilia mbali mgomo Jumatatu jioni.

Vile vile, inaaminika kuwa maafisa wa serikali walifanya mashauriano ya chini kwa chini na viongozi wa Kuppet, wakiwahakikishia kuwa matakwa yao yatatimizwa.