Siasa

Serikali imeoza – Azimio

January 31st, 2024 2 min read

NA BENSON MATHEKA

VINARA wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, wamehimiza Wakenya kutonyamaza huku serikali ya Kenya Kwanza ikiendeleza walichotaja kama maovu yanayowanyima riziki, haki na kuhujumu demokrasia ambayo nchi imekuwa ikifurahia kwa miaka mingi.

Wakisisitiza kuwa muungano huo ungali imara, vinara wenza wa muungano huo wa upinzani walilaumu serikali kwa maovu kama kuvuruga uhusiano wa Kenya na majirani wake, ukabila, ufisadi, kukandamiza raia kupitia gharama ya juu ya maisha kutokana ushuru unaolemea wengi, kuingilia mfumo wa haki na kuua demokrasia.

“Muungano umeridhika na kazi unayofanya ya kutetea Wakenya na unaahidi kuendelea kukosoa serikali na kuilaumu kwa kwa maovu kama kuendelea kuongeza ushuru, kudorora kwa uhusiano wa Kenya na majirani wetu, kiwango cha juu cha ufisadi, ukabila katika utumishi wa umma, kudharau utawala wa sheria, shilingi ya Kenya kupoteza thamani yake na kudorora kwa uchumi kwa jumla,” vinara hao walisema baada ya mkutano wa kwanza wa baraza lake kuu uliohudhuriwa na vinara wenza isipokuwa kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ambaye yuko nje ya nchi.

Katika taarifa iliyosomwa na kiongozi wa chama cha Narc-Kenya Martha Karua na mwenzake wa DAP-Kenya Eugene Wamalwa, vinara hao walisema hali ya ugumu wa maisha inachangiwa na sera za serikali na sio raia wa nchi hii, matukio mengine ulimwenguni au serikali iliyopita.

“Ni serikali ya Kenya Kwanza, sio watu wa Kenya wanaosababisha maovu haya ambayo yanawaumiza raia wa Kenya wasio na hatia,” alisema Bw Wamalwa.

Rais William Ruto na Naibu wake Rigathi Gachagua, wamekuwa wakiongoza washirika wao kulaumu utawala wa Rais (Mstaafu) Uhuru Kenyatta, vita vya Israeli na Hamas huko Gaza kwa kupanda kwa bei ya mafuta.

Vile vile, wamekuwa wakilaumu serikali ya Bw Kenyatta kwa kutumbukiza nchi katika madeni.

Muungano huo ulisema utawala wa Kenya Kwanza chini ya Rais Ruto umejaribu kugawanya vinara wake ili usiongoze Wakenya kuikosoa na kufichua maovu serikalini.

“Kwa sababu muungano umeweza kudumisha umoja wake, Wakenya wameamka, wamejua ukweli na kupata ujasiri wa kukosoa utawala huu. Wakenya wameamka hata katika maeneo ya mashambani ya nchi hii kukosoa serikali kwa kuwadanganya na kutowajali raia. Tunahimiza Wakenya kuendelea kuonyesha ujasiri na kukosoa serikali hii. Tunasimama na Wakenya wote kukomboa nchi yao,” walisema.

Mkutano wa Jumanne ulijadili mbinu na mikakati muhimu ya kutia nguvu Azimio ikiwa ni pamoja na vyama tanzu kujitia nguvu huku vikiendelea kukosoa serikali kwa pamoja kama muungano.

“Vyama vyote tanzu vimeahidi kuendelea na mpango wa pamoja wa kutatua changamoto zinazokumba nchi na pia kutetea na kulinda demokrasia,” alisema Bi Karua

Aliongeza: “Azimio iko imara na haiendi popote; imejitolea kushirikiana kuona kwamba, kuna uwazi na uadilifu serikalini, ushirikishaji wa umma, utawala bora, kuheshimiwa kwa katiba na utawala wa sheria, haki ya jamii na kukomesha ubaguzi.”

Vinara hao walisema baadhi ya hatua za serikali zinatishia kurudisha Kenya kuwa nchi ya chama kimoja cha kisiasa na kupalilia umaskini.

“Azimio inasikitishwa na kuongezeka kwa gharama ya maisha, ushuru unaozidi kuongezeka na usiofaa, kuvurugika kwa sekta ya elimu na kurejea kwa ufisadi wa wazi na wa hali ya juu,” alisema Bi Karua.

Waliohudhuria mkutano huo ni Raila Odinga, Bi Karua, Eugene Wamalwa, Mwangi wa Iria, Wycliffe Opranya, Peter Munya, Jeremiah Kioni, Nderitu Muriithi, George Wajackoyah, Opiyo Wandayi.