Habari Mseto

Serikali imetoa hatimiliki milioni 4.5 za mashamba – Uhuru

November 12th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

Serikali ya Jubilee imetoa hatimiliki milioni 4.5 kwa wamiliki wa ploti na mashamba nchini, tangu ichukue hatamu ya uongozi 2013.

Akipigia upatu hatua hiyo, Rais Uhuru Kenyatta amesema itasaidia kuangazia mizozo ya ardhi ambayo imekuwa ikishuhudiwa mara kwa mara katika baadhi ya maeneo nchini.

“Kufikia sasa serikali ya Jubilee imetoa hatimiliki milioni 4.5 kuanzia 2013, ikilinganishwa na hatimiliki zilizotolewa tangu Kenya ipate uhuru 1963 hadi tulipochukua usukani,” akasema Rais Kenyatta Alhamisi kwenye hotuba kwa taifa katika makao makuu ya bunge la kitaifa.

Akiahidi kuwa ataendelea kutoa hatimiliki zaidi, kiongozi huyo wa nchi alisema serikali inalenga kuimarisha mikakati ya utoaji huduma za mashamba, kwa kukumbatia mfumo wa kidijitali.

“Mbali na kutoa hatimiliki, tunataka huduma za ardhi na mashamba ziwe zinatolewa kwa njia ya kidijitali ili kupunguza kazi na muda na pia gharama ya juu,” akaelezea Rais Kenyatta.

Alisema huduma za ardhi na kutoa hatimiliki zikitekelezwa kwa njia ya kidijitali, visa vya ufisadi na unyakuzi wa ardhi katika idara husika zitaweza kukabiliwa.