Habari Mseto

Serikali imeweka zuio kwa manufaa yenu, Supkem yaambia wakazi Eastleigh na Mji wa Kale

May 8th, 2020 2 min read

Na CECIL ODONGO

BARAZA Kuu la Waislamu Nchini (Supkem) limeunga mkono hatua ya serikali kuweka kafyu ya kutotoka au kuingia katika mitaa ya Eastleigh na Mji wa Kwale kutokana na idadi kubwa ya maambukizi ya virusi vya corona katika maeneo hayo.

Mwenyekiti wa Supkem Hassan Ole Naado kupitia taarifa, amesema hatua hiyo ilichukuliwa ili kuzingatia maslahi ya kiafya ya wakazi wa mitaa hiyo.

Pia aliongeza kwamba hatua hiyo Itazima kuenea kwa virusi hivyo ambavyo vimesababisha vifo vya watu 29 nchini kwenye mitaa jirani.

Ikizingatiwa kwamba wengi wa wakazi wa maeneo hayo ni waumini wa dini ya Kiislamu, Bw Ole Naado amesema ni jukumu la Supkem kuhakikisha kwamba wanatii agizo la serikali bila purukushani zozote kushuhudiwa na pia wanaendelea na ibada zao nyumbani wakati huu wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe mnamo Jumatano alitangaza kufungwa kwa mitaa hiyo miwili kwa muda wa siku 15 ijayo kutokana na maambukizi mengi ya virusi vya corona miongoni mwa wakazi.

“Tunawasikitikia na kuwaombea walioathirika na hali hii hasa wakati huu wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan. Hata hivyo, Supkem inaishukuru serikali kwa kutoa fursa kwa wanaotoa huduma spesheli kuendelea na kazi zao. Tunawatilia dua na kuwaombea utulivu kipindi hiki mitaa hii miwili umefungwa,” akasema Bw Ole Naado.

Ikizingatiwa mitaa hiyo miwili hukumbwa na uhabe wa maji, afisa huyo ameirai serikali iwape nafasi wafanyabiashara wanaochuuza bidhaa hiyo kwa kutumia mikokoteni ndipo maisha ya wakazi yasitatizike.

“Tumepokea ripoti kwamba familia kadhaa zinakosa maji baada ya wachuuzi wa bidhaa hiyo adimu kugomea kazi wakihofia kuadhibiwa na maafisa wa polisi. Huenda janga la kibinadamu likatokea kwenye mitaa hii iwapo maji yatakosekana,” akaongeza.

Ingawa hivyo, Bw Ole Naado ameiomba serikali ishirikiane na Supkem na viongozi wa Kiislamu kwenye mitaa hiyo iwapo patatokea suala lolote lisiloridhisha badala ya kuwakabili raia kupitia maafisa wa usalama wanaoshika doria katika mitaa hiyo.