Habari

Serikali inatatizika kuwaua nzige – Kiunjuri

January 10th, 2020 2 min read

Na CECIL ODONGO

SERIKALI kupitia Wizara ya Kilimo imekiri Ijumaa inapata wakati mgumu kuwamaliza nzige wa jangwani ambao wamevamia kaunti 10 za Kaskazini Mashariki na Mashariki tangu mwisho wa mwaka 2019.

Juhudi zimekuwa zikiendelea kuwaangamiza wadudu hao hatari baada ya serikali kuanza kutumia ndege za angani kuwanyunyiza kemikali nyakati za mchana.

Waziri wa Kilimo, Bw Mwangi Kiunjuri alisema wadudu hao hutoka eneo moja hadi jingine kwa kasi ya kilomita 120 kwa siku. Kwa hivyo imekuwa vigumu kuwafuatilia ili kuwaua kwa kutumia kemikali hiyo.

Kwa mujibu wa Bw Kiunjuri, itakuwa tu rahisi kuwaua nzige hao iwapo jamii ya kaunti husika watawapasha wanaohusika na oparesheni maliza nzige kuhusu maeneo wanakojikusanya kulala nyakati za jioni au kabla ya kuamka asubuhi.

“Nataka kuwahakikishia Wakenya kwamba tunaendelea na juhudi za kuwamaliza nzige hao ambao uwepo wao umeathiri maisha ya wakazi. Ni vigumu kuwamaliza wakiwa wamepaa angani kama kundi. Alhamisi, rubani wa ndege inayotumika kunyunyiza dawa ya kuwaangamiza alilazimika kujiweka kwenye hatari na kupangusa dirisha la ndege ili kuona vyema,” akasema Bw Kiunjuri akiwahutubia wanahabari katika majengo ya bunge.

Wizara hiyo imepanga kuandaa mkutano wa wataalamu wa sayansi kutoka vitengo mbalimbali katika mji wa Isiolo ambapo mafunzo yatatolewa kwa wanaohusika na operesheni ya kuwatokomeza wadudu hao kisha nambari maalum ya kuwasiliana na wizara ikatolewa.

Aidha Bw Kiunjuri alipuuzilia mbali habari kwenye vyombo vya habari kwamba wadudu hao wameenea na kufikia kaunti ya Meru, akisema wananchi waliwaona nzige wa kawaida tu wala si nzige hao wa jangwani.

“Nimewasiliana na gavana wa Meru Kiraitu Murungi na nzige walionekana hao walikuwa wale wa kawaida wenye pembe ndefu. Nimemweleza kwamba jambo muhimu ni kuongea na wananchi na kutambua mkusanyiko wao ndipo tupashwe habari na kisha tufike kuwaua kwa urahisi,” akaongeza Bw Kiunjuri.

Kibarua kigumu zaidi hata hivyo ni kwamba ndege zinazonyunyiza kemikali haziwezi kuendesha oparesheni za kuwaliza wadudu hao nyakati za usiku huku ndege mbili zikipelekwa Isiolo na Wajir kusaidia katika juhudi za kuwaangamiza.