MakalaSiasa

Serikali inavyojenga wanasiasa ikidhani inawatia adabu!

August 23rd, 2020 3 min read

Na WANDERI KAMAU

HATUA ya polisi kuwakamata maseneta watatu Jumatatu na kuwazuia kushiriki kura muhimu kuhusu Mfumo wa Ugavi wa Mapato kwa Kaunti, imeendeleza “kosa” ambapo serikali imekuwa ikiwajenga viongozi wa kisiasa ikidhani inawaadhibu.

Maseneta Cleophas Malala (Kakamega), Steve Lelengwe (Samburu) na Dkt Christopher Langat (Bomet) walikamatwa katika hali tatanishi siku ambapo Seneti ilipangiwa kupiga kura kuhusu mfumo huo tata.

Lakini licha ya kukamatwa kwao, wadadisi wanasema kwamba badala ya kuwaadhibu, serikali iliimarisha nyota zao kisiasa, hasa baada ya mamia ya wakazi katika kaunti zao kujitokeza kuikashifu kwa “kuwahangaisha viongozi wao.”

Katika Kaunti ya Kakamega, mamia ya wafuasi wa Bw Malala walifanya maandamano makubwa mjini Mumias, wakimtaja kuwa “shujaa” na “kiongozi mzalendo.”

Baadhi ya vijana hata walifunga barabara na kuteketeza magurudumu kuonyesha ghadhabu yao. Hali ilikuwa vivyo hivyo katika kaunti za Samburu na Bomet, ambapo maelfu ya wafuasi wa maseneta walijitokeza kwa wingi kuwalaki, waliposafirishwa na polisi ili kufunguliwa mashtaka.

Wadadisi wanasema serikali “ilijikwaa” hasa baada ya viongozi hao kuachiliwa na baadhi ya mashtaka waliyokabiliwa nayo kufutiliwa mbali na Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji.

“Baadhi ya maseneta hao hawakujulikana na wengi kabla ya kukamatwa kwao. Serikali iliwapa umaarufu mkubwa kwa muda mfupi kwa kisingizio cha kuwaadhibu. Ni kosa ambalo limewahi kufanywa hapo awali,” asema Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Viongozi wengine wanaotajwa kufaidi kwa ‘adhabu’ walizopewa ni Naibu Rais William Ruto, Gavana Hassan Joho (Mombasa), wabunge wa mrengo wa ‘Tangatanga’ Ndindi Nyoro (Kiharu), Moses Kuria (Gatundu Kusini), Alice Wahome (Kandara), Kimani Ichung’wa (Kikuyu) kati ya wengine.

Ni mbinu ambayo pia Rais Uhuru Kenyatta na Dkt Ruto wanaelezwa kufaidi kwayo katika uchaguzi mkuu wa 2013 walipokabiliwa na mashtaka ya uhalifu wa kibinadamu katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Wadadisi wanasema kuwa ikizingatiwa kwamba viongozi hawa ni wanasiasa, huwa wanatumia kutengwa ama adhabu dhidi yao kunadi dhana ya maonevu ili kujizolea umaarufu miongoni mwa wananchi.

Wanasema hii ndiyo mbinu ambayo Dkt Ruto anatumia kuendesha kampeni yake kuwania urais 2022, japo kichinichini kupitia jumbe za vijana anaokutana nao katika makazi yake mtaani Karen, Nairobi.Dkt Ruto amekuwa akitengwa na Rais Uhuru Kenyatta kwenye shughuli nyingi za serikali, hasa harakati za kupambana na janga la virusi vya corona.

“Dkt Ruto amepata nafasi mwafaka kujijenga kisiasa, kwa kunadi dhana kuwa yeye ni kiongozi aliyetengwa. Hatua hii inachochea hisia za huruma kutoka kwa wafuasi wake,” asema Bw Muga.

Mnamo Ijumaa, Dkt Ruto alijitetea vikali kuhusu kutengwa kwake, akisema kuwa angalau wakati huu hatahusishwa na kashfa ya uporaji wa fedha za kukabili virusi vya corona.Inadaiwa mabilioni ya fedha zilizotolewa na wahisani kuisaidia Kenya kukabili janga hilo zimeporwa na baadhi ya maafisa wakuu serikalini na katika Wizara ya Afya.

“Angalau kwa mara ya kwanza, sitahusishwa na sakata ya uporaji wa fedha za corona. Acha niendelee kuwa mtazamaji tu serikalini,” akasema Dkt Ruto, kwenye ujumbe alioweka kwenye mtandao wake wa Twitter.

Wadadisi wanasema kauli hiyo inaashiria wazi kuwa anatumia kutengwa kwake kujijenga kisiasa.Mnamo Jumatatu, Dkt Ruto vile vile aliungana na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, kuwakashifu polisi kwa kuwadhulumu maseneta.

“Kilicho dhahiri ni kuwa Dkt Ruto anatumia kila nafasi anayopata kuonyesha kwamba yeye si sehemu ya serikali na ametengwa kabisa. Hivyo basi, yeye si miongoni mwa wale wanoendesha maovu ya sasa,” asema Prof Edward Kisiang’ani, ambaye ni mdadisi wa siasa.Mbinu hii pia iliwahi kutumiwa na Gavana Joho kati ya 2013 na 2017, kulipozuka tofauti kubwa za kisiasa kati yake na serikali ya Rais Kenyatta.

Kwa mujibu wa Bw Kazungu Katana, ambaye ni mchanganuzi wa siasa za Pwani, Bw Joho alitumia tofauti hizo kubuni dhana ya kuwa yeye ni “mtetezi wa Wapwani na maslahi yao.”

Anasema serikali ya Jubilee iliimarisha umaarufu wa Joho bila kujua, hasa alipozuiwa kuhudhuria baadhi ya hafla za Rais Kenyatta eneo la Pwani.“Joho aliibuka kuwa maarufu kwa kila mmoja, kwani alionekana kuwa mtetezi na sauti kuu ya Wapwani ambayo ilikuwa imekosekana kwa muda mrefu. Hiyo ndiyo moja ya sababu zilizomfanya kuchaguliwa tena kwa kishindo,” asema Bw Katana.

Katika eneo la Mlima Kenya, wabunge Nyoro, Kuria, Ichung’wa na Wahome wameibukia kuwa maarufu baada ya kunyang’anywa walinzi wao.Mwaka uliopita, Bw Nyoro alikamatwa na polisi makabiliano makali yalipozuka kati yake na mbunge maalum Maina Kamanda katika eneo la Gitui, Kaunti ya Murang’a.

Baadhi ya wenyeji waliandamana wakidai mbunge wao “alionewa.”Hata hivyo, wadadisi wanasema kuwa si kila wakati ambapo viongozi hufaulu kwa kutumia mbinu hii.

“Lazima viongozi wafahamu kwamba wananchi wanawatazama kwa karibu. Si kila mara ambapo mbinu hii hufaulu,” aonya Bw Felix Onyiego, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya utawala wa umma.