Serikali inavyokiuka Katiba kuacha raia wafe njaa

Serikali inavyokiuka Katiba kuacha raia wafe njaa

Na LEONARD ONYANGO

INAONEKANA haki zilizoorodheshwa kwenye Katiba zinalenga kuwafaa tu mabwanyenye na kubagua maskini.

Sura ya Pili ya Katiba imeorodhesha haki mbalimbali za Wakenya. Kifungu cha 43 (1) kinasema kuwa hakuna Mkenya anafaa kuhangaishwa na njaa na kila mtu anastahili kuwa na chakula cha kutosha na ubora wa juu.

Kifungu hiki hakijatekelezwa kwani tangu kupitishwa kwa Katiba ya sasa 2010, baa la njaa limesalia donda ndugu humu nchini.

Inasikitisha kwamba kila mwaka mamilioni ya Wakenya wanalazimika kula matunda machungu ya mwituni ili kunusuru maisha yao.

Ahadi ya Rais Kenyatta aliyotoa baada ya kuapishwa kwa muhula wa pili Novemba 28, 2017, kwamba angehakikisha nchi inazalisha chakula cha kutosha kabla ya kustaafu 2022, imesalia ndoto.Rais Kenyatta mapema mwezi huu, alitangaza baa la njaa kuwa janga la kitaifa.

Lakini kufikia sasa hakuna juhudi za kuridhisha kuhakikisha kwamna waathiriwa wa njaa wanapewa chakula cha kutosha.

Ni kinaya kwamba Wakenya wanahangaishwa kwa njaa ilhali wakulima katika eneo la Bonde la Ufa wamehifadhi maelfu ya magunia ya mahindi yaliyokosa wanunuzi kutokana na bei mbovu.

Takwimu za wizara ya Kilimo zinaonyesha Kenya ina hekta 1.3 milioni za ardhi ambayo inastahili kuwekwa miradi ya kilimo cha umwagiliaji maji.

Lakini ni asilimia 14 ya eneo hilo inatumika kuzalisha chakula. Hiyo inamaana kwamba serikali ikiongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji maji hadi asilimia 40, baa la njaa litazikwa katika kaburi la sahau humu nchini.

Kwa sababu njaa inahangaisha maskini hohehae, viongozi ambao wengi wao ni mabwanyenye, hawajali.Kifungu cha 43 pia kinasema kuwa kila Mkenya ana haki ya kuishi katika mazingira safi yaliyo na maji safi na salama.

Lakini wakazi wa maeneo yaliyokumbwa na ukame sasa wanalazimika kutumia pamoja na wanyama maji hivyo kuhatarisha afya zao.

Hali ya mazingira katika mitaa ya mabanda mijini pia ni mbovu lakini hakuna anayewajali; viongozi wanafanya kazi ya kuzunguka kila mahali wakisaka kura.

Kifungu cha 43 (2) kinasema kuwa hakuna Mkenya anafaa kunyimwa matibabu ya dharura.Mara kadhaa, tumesoma na kusikia habari kuhusu wagonjwa wanaonyimwa matibabu kwa kukosa hela.

Kifungu cha 43 (3) kinasema kwamba serikali itatoa msaada kwa watu wasio na uwezo wa kujisaidia pamoja na watu wanaowategemea.

Maelfu ya wazee, walemavu na mayatima wanahangaika bila msaada.Katiba haijasema ni hatua ipi inayofaa kuchukuliwa dhidi ya hospitali inayokataa kutibu mgonjwa anayehitaji matibabu ya dharura.

Katiba pia haijapendekeza adhabu yoyote dhidi ya maafisa wa serikali wanaolaza damu na kuacha watu wakihangaishwa na makali ya njaa au kukosa maji.

Wabunge hawana budi kubuni sheria itakayoziba mapengo hayo yaliyo katika Katiba kuhakikisha kuwa kila Mkenya anapata chakula na maji ya kutosha na kuishi katika mazingira safi.

You can share this post!

KINYUA BIN KINGORI: Vyama vya kisiasa vinavyoendesha...

Waislamu waenda Saudia kwa Umrah