Habari MsetoSiasa

Serikali itaagiza mahindi kutoka mataifa ya Comesa – Kiunjuri

July 17th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Kilimo Mwangi Kiunjuri amefafanua kuwa wizara yaka itaruhusu uagizaji wa mahindi kutoka mataifa jirani pekee wala sio kutoka Mexico kama inavyodaiwa.

Aliwaambaia wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Kilimo Jumatano kwa mahindi hayo ambayo pia yataagizwa kutoka mataifa wanachama wa Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) yataziba pengo la uhaba wa magunia milioni sita ya mahindi.

“Wizara itatoa nafasi kwa wafanyabiashara kuagizaji wa mahindi kutoka mataifa ya Uganda, Tanzania, Ethiopia na maataifa mengine wanachama wa COMESA wala sio Mexico inavyodaiwa,” Bw Kiunjuri akaiambia kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Mandera Kusini Adan Ali Haji.

“Nimekuwa nikisema kwamba bei ya unga imependa kutoka Sh90 hadi Sh124 kwa paketi moja ya kilo mbili kwa sababu kuna uhaba wa bidhaa hiyo nchini. Upungufu huo wa maguni milioni 6 utajazwa na mahindi kutoka mataifa jirani wala sio Mexico kama inavyodaiwa,” Bw Kiunjuri akaongeza.

Wiki jana Waziri huyo alinukuliwa katika vyombo vya habari akisema kuwa wizara yake itaagiza takriban magunia 12.5 milioni kutoka mataifa ya nje. Alisema hali hiyo inatokana na uhaba mkubwa wa bidhaa hiyo katika masoko ya humo nchini, hali ambayo imechangia kupanda kwa bei ya unga.

Tangazo hilo liliwakera wabunge wanachama wa kamati ya Kilimo inayoongozwa na Mbunge wa Mandera Kusini Adan Haji.Wabunge hao walidai kuwa kuna takriban magunia milioni nne (4) ya mahindi katika maghala ya Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) ambayo itatosheleza mahitaji ya kitaifa hadi msimu wa mavuno utakapoanza

“Uchunguzi wetu umebaini kuwa kuna jumla ya magunia 2.6 milioni ya mahindi katika maghala ya Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB). Kando na hayo wakulima na wasagaji unga bado wanashikilia jumla ya magunia 1.5 milioni ambayo kwa jumla yanatosheleza mahitaji yetu hadi Septemba,” Bw Haji akawaambia wanahabari katika majengo ya bunge Jumanne.

Wazo la Bw Kiunjuri pia lilipingwa na mwenyekiti wa Bodi ya Kusimamia Hazina ya Mahindi ya Kimkakati (SGRB) Dkt Noah Wekesa.

Dkt Wekesa alishikilia kuwa kuna mahindi ya kutosha nchini na hamna haja ya kuagiza mengine kutoka mataifa ya ng’ambo akisema hatua hiyo itaumiza wakulima ambao wataanza kuvuna mahindi mwishoni mwa mwezi wa Septemba.

“Uhaba ambao Waziri Kiunjuri anazungunzia ni wa kubuni wala sio halisi. Takwimu zetu kama bodi ni kwamba kuna takriban magunia milioni 4 ya mahindi nchini ambayo yanatosha hadi msimu wa mavuna utakapoanza Septemba,” akasema.

Wakati huo huo, Bw Kiunjuri jana alitangaza kuwa serikali imetenga Sh3.5 bilioni za kununua mahindi ya wakulima mwaka huu.