Habari

Serikali itaendelea kupiga jeki TVET, aahidi Rais Kenyatta

January 28th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta amekariri kujitolea kwa serikali yake kupiga jeki kuanzishwa kwa taasisi za kutoa mafunzo ya kiufundi (TVET) akisema mustakabali wa taifa utaongozwa na mafunzo kama hayo.

Rais amesema vyuo vya TVET vitawapa vijana ujuzi hitajika ambao utawawezesha kupata ajira au kujiajiri katika mazingira ya sasa yenye ushindani mkubwa.

“Hii ndiyo ilikuwa ndoto ya mababu zetu. Tulipotoka pale sote tulianza kuamini kuwa wale wenye shahada za digrii ndio watapata maisha mazuri siku zijazo, lakini ukweli ni kwamba nafasi nyingi za kazi zilizoko sasa ni zile zinazowapa nafasi ya kutumia talanta zao,” amesema Rais Kenyatta.

Akaongeza: “Hii ndiyo maana tumeweka msisitizo mkubwa kwa TVET ili iwape watu wetu ujuzi unaohitajika katika soko la ajira katika Karne hii ya 21. Hapa ndipo mahali tunahitaji kuwekeza.”

Kiongozi wa nchi ameongea Jumanne katika Ikulu ya Nairobi aliposhuhudia hafla ya kupokezwa kwa hatimiliki ya ardhi ya ukubwa wa ekari inayomilikiwa na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Kiambu (KIST) kwa Hazina ya Taifa na Bodi ya wasimamizi wa KIST.

Cheti hicho cha ardhi kimewasilishwa kwa Hazina ya Kitaifa kufuatia makubaliano yaliyofikiwa wakati Rais Kenyatta alizuru Ujerumani Aprili 2016 ambapo alipata ufadhili kutoka kwa serikali ya nchi hiyo kwa taasisi hiyo. Ujerumani inapanga kufadhili ujenzi wa mradi wa uhandisi kwa jina “mechatronics” katika KIST.

“Nilipozuru Ujerumani, nchi hiyo ilikubali kufadhili ajenda yetu ya TVET katika chuo cha KIST. Kwa sababu huu ni ufadhiliwa wa serikali, hitaji ni kwamba ardhi ambayo mradi huo utatekelezwa sharti imilikiwe na serikali,” akasema Rais Kenyatta.

Ujerumani ilikubali kufadhili mradi huo kwa kima cha Sh2.2 bilioni.