Serikali italipa fidia ya Sh14 bilioni kwa walioshambuliwa na wanyamapori – Balala

Serikali italipa fidia ya Sh14 bilioni kwa walioshambuliwa na wanyamapori – Balala

Na ALEX KALAMA

WAZIRI wa Utalii, Bw Najib Balala amehimiza Shirika la Wanyamapori (KWS), kujenga uhusiano mwema na jamii kwa kuihamasisha jinsi ya kuepuka mashambulizi kutoka kwa wanyamapori.

Hatua hiyo alisema itasaidia kupunguza mizozo kati ya binadamu na wakazi, ambapo visa hivyo vimesababisha vifo na majeraha.

“KWS tafadhalini wekeni juhudi za kuhakikisha kuna uwiano na jamii na muweze kuwafundisha watu wapate kuelewa namna ya kuishi na wanyama,” alisema Bw Balala.

Alisema kwa kipindi cha miaka mitatu, serikali ya kitaifa imetumia takriban Sh2 bilioni kulipa fidia kwa wananchi walioashambuliwa na wanyamapori nchini.

Akizungumza na wanahabari katika eneo la Watamu, Kaunti ya Kilifi, Bw Balala alisema jumla ya fedha zinazostahili kulipwa wananchi walioathirika kutokana na mashambulizi ya wanyama ni Sh14 billioni.

“Pesa zilizopaswa kulipwa kama fidia kwa jamii zilizoathirika na mashambulizi ya wanyamapori ni Sh14 bilioni ila kufikia sasa ni Sh2 bilioni pekee ambazo serikali imelipa fidia kwa wananchi,” alisema Bw Balala.

Aliongeza, “Watu wanaoishi karibu na wanyama wanafaa kuwa waangalifu zaidi ili kuepuka kutokea kwa visa kama hivi. Lazima tuweke mikakati ya kupunguza shida hizo.”

Ni kauli ambayo imeungwa mkono na mkurugenzi mkuu wa shirika la KWS, Bw John Migui Waweru.

Bw Waweru alisisitiza haja ya gharama hizo kupungua huku akidokeza kuwa tayari wanaendelea kutoa hamasa katika jamii ili kuepusha mizozano kati ya binadamu na wanyama.

‘Gharama itapungua na tungependa kuiona ikipungua lakini wale wananchi ambao wanaishi na wanyama lazima waelewe kuwa kuna mbinu zile ambazo wanaweza kuishi,’ alisema Bw Waweru.

You can share this post!

Ruto afaulu kunusuru UDA baada ya mzozo kutatuliwa

Waganga waonywa dhidi ya kutibu wasichokielewa