Habari MsetoSiasa

Serikali itazidi kujitolea kumpa kila mtoto elimu ya msingi – Rais

May 21st, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta amesema Serikali itasalia imara katika juhudi zake kabambe za kuhakikisha watoto wote wa Kenya wanapata elimu ya msingi.

Kiongozi wa taifa alisema serikali yake itaendelea kuwekeza katika miradi ya upanuzi wa miundo msingi katika shule zote za msingi na za upili kama njia ya kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanasoma katika mazingira faafu.

Rais Kenyatta alisema hayo Jumanne katika Ikulu ya Nairobi alipoikabidhi Shule ya Upili ya Wasichana ya Kamacharia basi lenye uwezo wa kubeba abiria 52.

“Nawahimiza kutia bidii masomoni wakati huu ambapo serikali yangu inajizatiti kuwekeza pesa nyingi katika sekta ya elimu. Hatua hii inachukuliwa kwa lengo la kuhakikisha kuwa watoto wote nchi wanapata nafasi ya kupata elimu ya msingi,” akasema.

Rais Kenyatta alitumia fursa hiyo kutoa changamoto kwa wanafunzi kote nchini kutia bidii masomoni na kuepuka mienendo potovu ikiwemo uhusiano wa kimapenzi.

“Tieni bidii na muwe wakakamavu. Mnayo safari ndefu. Na hivyo hakuna haja ya kuwa na haraka ya kuingilia mambo ya anasa na tabia mbovu. Lengeni masomo pekee,” akawashauri.

“Zawaidi hii inalenga kuwatia shime msome kwa bidii ili muandikishe matokeo bora mwishoni mwa mwaka,” Rais Kenyatta akawaambia wanafunzi hao wa shule ya upili ya Kamacharia

Mbali na kuwakabidhi basi hilo, Rais Kenyatta pia alitoa miche ya miti ya kiasiili kwa wanafunzi hao kwa ajili ya kupandwa huku akiwahimiza wanafunzi hao kutunza mazingira..

Mbunge wa Mathioya Peter Kimari Kihara, aliyeandamana na wanachama wa bodi ya shule, walimu na wanafunzi ,alimpongeza Rais kutokana na miradi inayoendelea katika eneo lake la uwakilishi bunge.

Alitoa mfano wa miradi iliyokamilika na ile inayondelea katika eneo bunge lake ikimwemo barabara na uunganishaji umeme iliyoanzishwa katika kipindi cha uongozi wa Rais Kenyatta.

Mbunge huyo alimpongeza Rais Kenyatta kutokana Sh150 zilizotengwa na Serikali ya Kitaifa kwa ukarabati wa Taasisi ya Kiufundi ya Mathioya akisema taasisi hiyo ni muhimu kwa hali ya baadaye ya vijana katika eneo hilo.