Habari

SERIKALI: Kazi kwenu vijana

April 5th, 2020 2 min read

Na JUMA NAMLOLA

SERIKALI sasa inawaomba vijana wawe kwenye mstari wa mbele kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona. Waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe Jumamosi aliwataka vijana watumie nguvu zao kuhamasisha jamii pamoja na kuleta mabadiliko ya maana kwenye juhudi za kuzuia Corona kusambaa nchini.

“Natoa ombi maalumu kwa vijana wetu ambao ndio sehemu kubwa ya jamii. Takwimu zinaonyesha kuwa vijana ndio wanaoambukizwa virusi kwa wingi na wanavisambaza kwa wazee na wakongwe,” akasema.

Aliwahimiza wachukue hatua za kuhakikisha hawaendelei kusambaza virusi hivyo kupitia tabia yao ya kutojali.

“Najua vijana damu inawachemka na wanafurahia kusafiri hapa na pale. Nawaomba msijipeleke mashambani, kwa sababu kwa kuenda huko, mnaweza kuwaua wazazi au babu na nyanya zenu,” akasema.

Badala yake, waziri anawataka vijana watumie mikakati na nguvu zao za kujiweka katika makundi kushawishiana na kufanya shughuli zinazoweza kumaliza kabisa maambukizi hayo, ambayo kufikia jana yameathiri watu 126 nchini.

“Tunajua haitakuwa rahisi, itakuwa ngumu. Hii si safari ambayo mnatarajiwa kuimaliza peke yenu. Ni jukumu lenu kama vijana kuliokoa taifa hili. Mungu kwa hekima zake ameamua kuwa nyinyi muwe hai wakati huu ambapo nchi inahitaji vijana, ili mchukue jukumu la kumaliza ugonjwa huu,” akasema.

Bw Kagwe aliwakumbusha vijana kwamba, kama ambavyo katika historia kulikuwa na vijana waliopigania uhuru na wengine wakaleta mageuzi, vijana wa sasa ni nafasi yao kumaliza corona.

Kauli hiyo ya Bw Kagwe ina maana kuwa, vijana wanapaswa kuwajiika kwa makosa watakayofanya, yatakayosambaza virusi hivyo nchini. Takwimu za wizara ya Afya zinaonyesha kuwa, asilimia kubwa ya watu walioambukizwa corona nchini ni watu wa chini ya miaka 35.

Katika baadhi ya maeneo ya nchi, vijana wengi bado wanashiriki michezo ya kuwaleta karibu kama vila Kamari. Wengine wanasafiri kutoka mji mmoja hadi mwingine au kuzuru mashambani, jambo ambalo linachangia kwa wingi usambazaji wa virusi.

Jana, waziri alionya kuwa, iwapo vijana wataruhusu uchumi wa nchi uathiriwe na virusi hivyo, ni wao watakaoumia zaidi.

“Msipoiokoa nchi, hakutakuwa na ajira na uchumi utaanguka. Ni nyinyi mtakaotuzika siku kwa mamia. Suluhisho kwa tatizo hili mnalo. Mkitaka, mnaweza kujipanga na kuzuia watu kukaribiana, miongoni mwa kanuni tulizotangaza,” akasema Bw Kagwe.

Kati ya watu 372 waliopimwa, wanne walipatikana kuwa na virusi hivyo.

“Wanaume wawili na mwanamke mmoja, wameambukizwa. Wawili walisifiri kutoka Malawi na Pakistani mtawalia,” akasema.

Waziri pia alizima mpango wa Idara Simamizi ya Nairobi kuwakusanya zaidi ya watu 600 katika jumba la Mikutano ya Kimataifa la Kenyatta (KICC) Jumatatu.