Habari

Serikali kuagiza magunia milioni nne ya mahindi kuepusha njaa

March 31st, 2020 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

SERIKALI imeidhinisha uagizaji wa magunia milioni nne ya mahindi kutoka nchi za nje ili kuzuia baa la njaa wakati dunia inapoendelea kupambana na virusi vya corona.

Waziri wa Kilimo, Bw Peter Munya Jumanne alisema magunia hayo yatajumuisha milioni mbili ya mahindi meupe ya utengenezaji unga wa ugali, na mengine milioni mbili ya kutengeneza lishe ya mifugo.

Wiki iliyopita, mwenyekiti wa Hifadhi ya Chakula nchini (SFR), Dkt Noah Wekesa akisema kuwa maghala ya serikali hayana chakula.

Dkt Wekesa alisema kuwa serikali iliuza magunia yote milioni 4 mwaka jana na kufikia sasa haijanunua mahindi mengine kutoka kwa wakulima.

Bw Munya aliwahakikishia Wakenya kuwa kuna chakula cha kutosha nchini huku akisema serikali imeweka mikakati kabambe ya kukabiliana na uhaba ambao huenda ukajitokeza kufuatia janga la virusi vya corona.

Aliwataka Wakenya kukoma kununua chakula kwa pupa kutokana na hofu kwamba huenda kikawa adimu katika siku za usoni.

Waziri Munya alionya kuwa maafisa wa wizara yake watakuwa wakizunguka katika masoko mbalimbali kunasa wafanyabiashara wanaouza vyakula kwa bei ya juu.

“Nawahakikishia Wakenya kwamba kwa sasa kuna chakula cha kutosha na watu wasinunue vyakula kwa pupa wakidhani kwamba kutakuwa na uhaba. Kununua vyakula kwa bei kutasababisha mfumko wa bei ya bidhaa muhimu. Tunawaonya wafanyabiashara watakaoongeza bei ya vyakula kuwa wataadhiniwa,” akasema Bw Munya.

Wizara ya Kilimo pia iliwataka wakulima kuendelea kuuza mazao yao kwa Bodi ya Mazao na Nafaka (NCPB) ili kuwezesha maghala ya serikali kuwa na chakula cha kutosha.

Wakulima sasa wanauza mazao yao kwa kampuni za kibinafsi za kusaga unga kwa bei ya juu.

Kuzuiliwa kwa shughuli za usafiri katika mataifa mbalimbali yanayokuza mahindi kwa wingi na janga la nzige ambalo limeathiri maeneo kadhaa humu nchini pia yamezua hofu ya kutokea kwa baa la njaa humu nchini.

Tayari Shirika la Chakula Duniani (FAO) limeonya kuwa huenda kukatokea kwa njaa duniani iwapo mikakati haitawekwa kuhakikisha kuwa shughuli za kilimo zinaendelea licha ya kuwepo kwa janga la virusi vya corona.