NJENJE: Serikali kuagiza mahindi kudhibiti bei ya unga iliyogonga Sh150

NJENJE: Serikali kuagiza mahindi kudhibiti bei ya unga iliyogonga Sh150

NA WANDERI KAMAU

KENYA inapanga kuanza kuagiza mahindi kutoka nchi zilizo nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ili kudhibiti bei za juu za unga zinazoshuhudiwa nchini.

Kwa sasa, pakiti ya kilo mbili za unga inauzwa kwa Sh150 kiwastani.

Waziri wa Kilimo Peter Munya alisema kuwa hatua hiyo inalenga kuwapa afueni Wakenya, ambapo wengi wanalazimika kutumia fedha nyingi kugharimikia chakula ili kulisha familia zao.

Alisema hatua hiyo pia inalenga kuwasukuma wafanyabiashara walioficha mahindi kuyatoa katika maghala yao na kuanza kuyauza.

Hata hivyo, alieleza kuwa uamuzi wa ni lini ambapo mahindi hayo yataanza kuingizwa nchini “utafanywa katika siku kadhaa zijazo.”

Serikali inasema kuwa shehena moja ya mahindi itakuwa ikitarajiwa kuwasili nchini kwa muda wa siku 45 baada ya kuagizwa kutoka nchi husika.

“Huenda akiba yetu ya mahindi ikaisha kwa muda wa miezi michache ijayo. Ili kudhibiti bei ya unga, kuna haja tuanze kuagiza mahindi hayo kutoka nchi za nje,” akasema Bw Munya.

Hii ni mara ya kwanza ambapo Kenya itakuwa ikiagiza mahindi kutoka nje ya ukanda wa EAC tangu mwaka 2017.

Alisema kuwa mahindi hayo yatakuwa yakiagizwa tu kulingana na kiwango kinachohitajika, ili kuepuka uagizaji wa mahindi mengi kuliko yanayohitajika na wafanyabiashara walaghai.

Bei ya gunia la kilo 90 la mahindi imeongezeka kutoka Sh2,800 na Sh3,700 mnamo Desemba na Machi mtawalia hadi Sh4,500 mwezi huu.

Kulingana na takwimu kutoka wizara, wakulima walikuwa wakishikilia jumla ya magunia 8.5 milioni ya mahindi kati ya magunia 10.1 milioni yaliyozalishwa. Ni hali ambayo imewaacha wasagaji wengi na uhaba mkubwa wa mahindi.

Takwimu zilionyesha kuwa wasagaji na wauzaji mahindi wana jumla ya magunia 1.5 milioni pekee. Halmashauri ya Kitaifa ya Kununua Nafaka (NCPB) haina mahindi yote kwa sasa.

Waziri alisema kuwa wauzaji mahindi wengi kutoka Uganda (ambako ndiko tegemeo la Kenya) wanauza zao hilo nchini Sudan Kusini kutokana na bei nzuri ikilinganishwa na Kenya.

  • Tags

You can share this post!

UJASIRIAMALI: Ugonjwa wa lupus haujamzuia kusaka riziki...

Arsenal yapoteza tumaini

T L