Habari Mseto

Serikali kuamua kuhusu mitihani baada ya mashauriano

June 15th, 2020 2 min read

Na BENSON AMADALA

WAZIRI wa Elimu George Magoha sasa amesema kuwa serikali inafanya mashauriano na washikadau mbalimbali kuhusu wakati ambapo watahiniwa watafanya mitihani yao ya Kidato cha Nne (KCSE) na Darasa la Nane (KCPE).

Prof Magoha amekuwa akisisitiza kuwa mitihani hiyo ya kitaifa haitaahirishwa.

Prof Magoha, aliyekuwa akizungumza katika Shule ya Msingi ya Kakamega jana, alisema kuwa ameridhishwa na maandalizi ambayo yanafanywa na shule mbalimbali katika juhudi za kuzuia maambukizi miongoni mwa wanafunzi shule zitakapofunguliwa kuanzia Septemba, mwaka huu.

Alisema kuwa kila mwanafunzi atapewa barakoa na dawa ya kuua viini ili kuwakinga dhidi ya kupatwa na virusi vya corona.

Prof Magoha alizitaka bodi zinazosimamia shule na wahisani kuunga mkono juhudi za serikali kuhakikisha kuwa wanafunzi wanawekewa mazingira salama shuleni watakaporejelea masomo yao.

“Tunaendelea kujadiliana na washikadau mbalimbali kuhusu suala hili la kufungua tena shule. Wiki chache zijazo tutaruhusu Wakenya wote kutoa maoni yao kabla ya serikali kutoa uamuzi wake wa mwisho,” akasema Prof Magoha.

Alisema uamuzi wa mwisho kuhusu ikiwa shule zitafunguliwa utatolewa baada ya kupata ushauri kutoka kwa wizara ya Afya na idara nyinginezo za serikali zinazohusika katika vita dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.

“Kwa sasa ninakagua shule ili kuona maandalizi yalivyo. Lakini kufikia sasa nimeridhishwa na maandalizi yaliyowekwa. Shule zimewekewa maji safi ya wanafunzi kunawa na mpangilio kuhusu wanafunzi watakavyoketi unaridhisha,” akasema Waziri Magoha.

Waziri wa Elimu aliyefanya ziara ya ghafla katika shule hiyo ya Kakamema, ambayo ilipoteza wanafunzi 15 katika mkanyagano mnamo Februari mwaka huu, alisema kuwa wabunge kote nchini wamesaidia pakubwa katika kusambaza tenki za maji shuleni.

Waziri aliwataka wabunge wa Teso Kaskazini na Teso Kusini kuunga mkono juhudi za serikali za kuhakikisha kuwa watoto wanalindwa dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona shule zitakapofunguliwa kwa kuwawezesha kupata maji ya kunawa.

“Viongozi wa Teso wanafaa kuiga wenzao katika maeneo mengineyo nchini,” akasema.

ambao wamekuwa wakisambaza matenki ya maji shuleni. Matenki hayo yatasaidia wanafunzi kunawa, hivyo kupunguza uwezekano wao kuambukizwa virusi vya corona,” akasema Prof Magoha.