Habari Mseto

Serikali kuchunguza kukatika kwa huduma za M-Pesa

December 10th, 2018 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT) Joe Mucheru ameagiza Mamlaka ya mawasiliano (CA) kushirikiana na Benki Kuu ya Kenya (CBA) kuchunguza kiini cha kukatika kwa huduma za Mpesa mnamo Jumamosi na Jumapili.

Katika taarifa yake, Waziri Mucheru alisema wizara yake imesikitishwa na kutatizika kwa huduma za M-pesa ambazo hutegemewa na maelfu ya Wakenya kila siku.

Alisema baada ya mamlaka ya CA na Benki Kuu kukamilisha uchunguzi wake watawasilisha ripoti yao kwa serikali. Ripoti hiyo itajumuisha mapendekezo ambayo kampuni ya Safaricom inayomiliki M-pesa unastahili kutekeleza ili kuepuka kutatizika kwa huduma hizo katika siku za usoni.

Waziri Mucheru, hata hivyo, aliwataka watumiaji wa M-pesa kuwa na laini mbadala ili kuepuka kutatizika huduma za Safaricom zinapokwama.

“Hata tunapohakikisha kwamba kampuni za kutoa huduma za mawasiliano ya simu zinahudumia wananchi bila kukwama, tunahimiza wateja kuwa na laini mbadala ili kuepuka changamoto sawa na hizo,” akasema Bw Mucheru.

Alisema kuwa Wakenya sasa inawezekana kwa Wakenya kutuma pesa kupitia laini ya kampuni yoyote ya kutoa huduma ya mawasiliano ya simu. Kampuni ya Safaricom Jumamosi ilikiri kuwa huduma zake za M-pesa zilikuwa na hitilafu.

Kampuni hiyo ya mawasiliano ilisema kuwa mtambo wake wa kuhifadhi data za M-pesa ulikuwa na matatizo.

“Tunasikitika, tunafahamisha wateja wa M-pesa kuwa huduma zetu sasa hazipatikani kutokana na hitilafu ya mitambo ya kielektroniki.”

Wahandisi wetu wanashughulika kuhakikisha kuwa huduma zinarejea,” ikasema taarifa ya Safaricom.

Kukatika kwa huduma za M-pesa kulizua hisia mbambali miongoni mwa Wakenya katika mitandao ya kijamii.

“Kutegemea Mpesa kwa muda mrefu kumenifanya kusahau nambari ya siri ya ATM. Nilienda kutoa fedha na nilisimama kando ya mtambo wa ATM nikijaribu kufikiria nambari ya siri,” akasema Ahmed Mohamed katika mtandao wa Twitter.

?Naye Fred Indimuli alisema kuwa ni hatari kuachia kampuni ya kibinafsi kuendesha uchumi wa nchi.

? “Inasikitisha kuwa kampuni ya Safaricom ilisitisha huduma zake bila kutoa taarifa kabla. Haifai kabisa,” akasema Kinuthia Pius.