Serikali kufanya mageuzi katika kilimo cha viazi

Serikali kufanya mageuzi katika kilimo cha viazi

Na WAIKWA MAINA

HATIMAYE Serikali ya Kitaifa imesikia kilio cha wakulima wa viazi nchini huku mageuzi yakitarajiwa yatakumbatiwa katika sekta hiyo ya kilimo mwaka huu.

Mageuzi hayo ni kama yale yaliyotekelezwa kwenye sekta ya kilimo cha kahawa na majani na yataanza mnamo Juni. Serikali kufikia mwezi huo itaweka marufuku dhidi ya uagizaji wa viazi mbatata huku jopo la kutekeleza mabadiliko katika sekta hiyo likitarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.

Wizara ya Kilimo itashirikiana na kaunti ambazo zinakuza viazi na sekta nyingine ili kuboresha kilimo cha viazi.

“Kwa miaka mingi tumekuwa tukila viazi na bidhaa nyingine zinazotokana na viazi vilivyokuzwa hapa nyumbani. Wageni wanaotoka nje ya nchi wamekuwa wakila vyakula vinavyotengenezwa na viazi.

“Hakuna sababu ya mtu yeyote kuagiza viazi kutoka nje ya nchi ila pale tu kutakapokuwa na uhaba. Viazi vyetu huwa ni bora zaidi na hata vinaweza kuuzwa nje ya nchi,” akasema Waziri wa Kilimo Peter Munya hivi majuzi.

Bw Munya alifichua kuwa wizara yake imeshauriana na wafanyabiashara kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu kilimo cha viazi kisha wakakubaliana kuhusu kusaka soko ndani na nje ya nchi.

“Wakulima watatuambia kile ambacho serikali inafaa kufanya, aina ya mbegu wanazotoka na jinsi zitakazokuzwa kisha kusafirishwa. Tutashauriana na Gavana wa Nyandarua Francis Kimemia kuhusu kubuniwa kwa jopo na wanachama wake kwa sababu kaunti yake ndiyo inayoongoza katika kilimo cha viazi,” akaongeza Bw Munya.

Kwa upande wake, Gavana Kimemia alisema jopo litakalobuniwa litasaidia kutatua changamoto kama ukosefu wa soko na pia vipimo bora na bei ya kila gunia la kilo 50. Pia litahakikisha kuwa wakulima wanapewa pembejeo za kilimo jinsi tu inavyotekelezwa kwa wakulima wa majanichai.

“Jopo hilo liibuke na bei bora ya kila kilo 50 za viazi. Waziri Munya anafaa kuwashirikisha magavana wote wanaotoka kaunti ambazo kilimo cha viazi kimeshamiri ili mapendekezo yatakayotolewa na jopo hilo yatekelezwe kikamilifu,” akasema Bw Kimemia.

Wakulima nao wamekuwa wakilalamikia changamoto kadhaa ambazo zimekuwa zikikumba kilimo cha viazi huku wengi wakilemewa na umaskini licha ya kujituma sana kila msimu.

Mkulima Geofrey Mwaniki, amesalia na magunia 70 ya viazi kutokana na bei duni sokoni. Alikuwa akiuza gunia moja la kilo 50 msimu wa Krismasi na mwaka mpya kwa Sh1,500 ila bei hiyo sasa imepungua hadi Sh800.

Alishangazwa na tukio la juzi ambapo KFC ililalamikia uhaba wa viazi ilhali wakulima wengi kama yeye kutoka Nyandarua wana viazi vingi ambavyo havijauzwa kutokana na ukosefu wa soko.

Kauli yake imeungwa mkono na Edith Wambui kutoka Njambini, eneobunge la Kinangop na Faith Wa Kepha ambao pia wameiomba serikali itekeleze mageuzi makubwa katika sekta hiyo ya mauzo ya viazi.

  • Tags

You can share this post!

Raila kifua mbele Pwani akiungwa mkono na magavana watano

Serikali yaagiza uchunguzi ufanywe kuhusu unyakuzi wa...

T L