Serikali kufunga shule za msingi za mabweni

Serikali kufunga shule za msingi za mabweni

WIZARA ya Elimu imetangaza mpango wa kupiga marufuku shule za mabweni kwa wanafunzi wa Gredi ya Kwanza hadi Tisa.

Katibu Dkt Belio Kipsang alisema ni muhimu kwa wanafunzi hao kuwa karibu na wazazi na walezi wao.

Akizungumza katika ufunguzi rasmi wa kongamano la 18 la Walimu Wakuu wa Shule za Msingi (KEPSHA) katika shule ya Sheikh Khalifa Bin Zayed jijini Mombasa, Dkt Kipsang alisema serikali itatumia shule za kutwa kwa masomo ya msingi na Sekondari Tangulizi (Junior Secondary).

“Hii ndiyo njia ya pekee ya kutangamana na watoto wetu. Naomba wazazi wawaongoze wana wao kwani wao ndio walimu wa kwanza. Ni jukumu ambalo hatuwezi kukwepa.,” alitanguliza Katibu.

“Tunasaidiana na walimu kulea watoto wetu. Hatuwezi kuwaachia walimu kazi yote,” akaongeza.

Dkt Kipsang alieleza kuwa wasimamizi wa shule za msingi wanapaswa kuelewa majukumu yanayotokana na kuwepo kwa sekondari za chini katika shule zao za msingi.

“Tuanze kutathmini uwezo wa shule zetu kuwa na sekondari hizi za chini. Iwapo kuna majukumu ambayo shule yako haiwezi kutekeleza, shule jirani itasaidia,” alieleza.

“Tutafundisha watoto sayansi ya msingi. Hivyo, tutalazimika kutumia maabara zetu kwa pamoja,” akaongeza afisa huyo wa ngazi ya juu katika Wizara ya Elimu.

Hatua ya kuondoa shule za bweni hasa kwa wanafunzi wa Sekondari Tangulizi, huenda ikawa pigo kwa wazazi ambao walipanga kuwapeleka wana wao shule za bweni.

Mwenyekiti wa Muungano wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi (KEPSHA) Johnson Nzioka ahutubu jijini Mombasa kwenye kongamano. PICHA | KEVIN ODIT

Ingawa hivyo, wakuu wa shule wamepongeza hatua ya serikali wakisema kuwa wazazi na walezi sasa watalazimika kuwajibika.

“Tunapongeza Wizara ya Elimu kuondoa shule za mabweni. Hii itahakikisha kuwa wanafunzi wako karibu na wazazi wao. Watoto hawa ni wadogo sana na wanahitaji kufuatiliwa kwa karibu,” akasema Bi Alice Kabeka, mwalimu wa Shule ya Msingi ya Baguo iliyoko Malindi.

Mwalimu Mkuu Bi Anne Babu wa Shule ya Gathonga, Kaunti ya Tharaka Nithi, akiunga mkono uamuzi huo aliomba maelezo zaidi.

“Hata hivyo, tunataka mwelekeo zaidi. Kuna wazazi walikuwa wamejiandaa kuleta wana wao katika shule zetu. Mabweni haya yatakwenda wapi?” akasema Bi Babu ambaye wengi wa wanafunzi 350 katika shule yake ni wanaoishi humo.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya wasichana ya Ryururu iliyo katika Kaunti ya Meru, Bi Rosemary Nyong’o, alielezea hofu ya kufungwa kwa shule zao kwa kukosekana kwa wanafunzi.

“Hatua hiyo ni nzuri. Shida ni kuwa, wanafunzi wanapopelekwa katika shule za kutwa, tutalazimika kufunga shule zetu,” akaeleza Bi Nyong’o.

Kongamano hilo la walimu wakuu limepangiwa kuendelea hadi Ijumaa.

Dkt Kipsang alitoa hakikisho kuwa serikali itashirikiana na wadau wote ili kuhakikisha kila shule ina rasilimali na miundomsingi ya kutosha, hasa katika utekelezaji wa mfumo wa CBC.

Aliwataka walimu wakuu kuweka rekodi za wanafunzi wote inavyofaa ili serikali ijue kuhusu mahitaji yanayofaa kushughulikiwa.

  • Tags

You can share this post!

Kampuni ya bima, Aga Khan kutoa matibabu ya bure

Ushindi wangu wa Agosti 9 ulikuwa wa haki, asisitiza Lenku

T L