Habari Mseto

Serikali kugharimia mazishi ya afisa wa GSU aliyeuawa DusitD2

January 23rd, 2019 1 min read

Na Leonard Onyango

Serikali itagharamikia mazishi ya afisa wa GSU aliyeuawa katika shambulio la kigaidi hotelini Dusit D2 Jumanne iliyopita.

Serikali Jumanne ilituma wafungwa kutoka magereza ya Manyani na Wundanyi kwenda kumjengea nyumba Japheth Ndunguja Nuru katika eneo la Kimala –Ndiweni mjini Taveta.

Awali, Wakenya waliisuta serikali baada ya familia ya shujaa huyo kuchangisha fedha kwa ajili ya mazishi.

Kupitia tangazo lililochapishwa gazetini jana, familia ya Japheth Ndunguja Nuru, aliyefariki akiwa na umri wa miaka 28, iliwataka wasamaria wema kutuma mchango wao kwa akaunti 566010 kwa ajili ya maandalizi ya mipango ya mazishi.

Familia ya afisa huyo aliyekuwa akihudumu katika Makao Makuu ya GSU Ruaraka, Nairobi pia ilisema itakuwa na mkutano wa kuchangisha fedha leo katika ukumbi wa ACK wa Kanisa la All Saints Cathedral.

Kulingana na tangazo hilo, Japheth atazikwa Jumamosi kijijini Kimala, Taita katika Kaunti ya Taita Taveta.

Nuru alikuwa miongoni mwa watu 21 waliouawa na magaidi katika shambulio lililotekelezwa katika hoteli ya Dusit D2.