Habari Mseto

Serikali kujenga vyoo kwenye mbuga ‘kuvutia watalii zaidi’

April 5th, 2024 1 min read

NA STANLEY NGOTHO

SERIKALI kuu itajenga vyoo vya kisasa na sehemu za kupumzika katika mbuga ya wanyamapori ya Amboseli ili kukuza utalii katika kaunti ya Kajiado, asema Waziri wa Utalii na Wanyamapori, Dkt Alfred Mutua.

Akizungumza katika Hifadhi ya Kitaifa ya Amboseli, Kaunti ya Kajiado Kusini, wakati wa gwaride la kufuzu kwa Walinzi wa wanyamapori wa Kaunti hiyo, Dkt Mutua alisisitiza kuwa uwepo wa vyoo katika mbuga hizo umepuuzwa kwa miaka mingi lakini ni muhimu kwa ustawi wa watalii.

“Tutajenga vyoo katika mbuga ili kuhakikisha watalii hawalazimiki kukimbilia hotelini mwao au kujisaidia vichakani. Tunataka wafurahie safari zao huku tukichuma pesa nyingi za kigeni,” Dkt Mutua alisema.