Serikali kujengea wahasiriwa Laikipia makazi

Serikali kujengea wahasiriwa Laikipia makazi

Na STEVE NJUGUNA

SERIKALI imeanza kuwajengea nyumba wakazi wa Ol Moran, kitovu cha ghasia zilizogubika kaunti ndogo ya Laikipia Magharibi, Kaunti ya Laikipia.

Tayari kituo cha polisi kimeanza kujengwa eneo hilo alivyoahidi Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i.

Nyumba za mamia ya familia katika eneo hilo ziliteketezwa katika msururu wa mashambulio ambayo yamedumu kwa muda wa zaidi ya wiki mbili.

Waziri Matiang’i aliyerejea Laikipia kwa siku ya pili jana Jumamosi, alitangaza kuwa serikali itafadhili ujenzi wa nyumbani zilizoteketezwa na majangili katika vijiji vilivyoko Ol Moran, Dam Samaki na Kisii Ndogo.

Alisema kila mmoja wa waathiriwa hao atajengewa nyumba yenye vyumba vitatu.

“Waathiriwa watafaidi kutokana na nyumba bora, kila mmoja. Kwanza, tutajenga nyumba 26 ambazo zitajengwa kwa mtindo sawa kabla ya kujenga nyingine 25,” akasema Dkt Matiang’i akiwa kijiji cha Kisii Ndogo.

Tangazo hili linajiri siku moja baada ya serikali kubuni eneo jipya la utawala katika kaunti hiyo kwa lengo la kudhibiti visa vya utovu wa usalama.

Tarafa ya Ol Moran ilibuniwa kutoka Kaunti-ndogo ya Laikipia Magharibi huku tarafa ya Ng’arua ikinyofolewa katika Kaunt-ndogo ya Nyahururu ili kuunda Kaunti-ndogo ya Kirima.

Makao makuu ya Kaunti ndogo mpya ya Kirima yatakuwa katika mji wa Ol Moran. Jumamosi, Dkt Matiang’i alisema polisi 100 zaidi watatumwa katika kituo kipya cha polisi.

“Tayari Naibu Kamishna wa Kaunti (DCC) ameripoti katika kaunti-ndogo mpya. Maafisa wengine wa serikali wakiwemo maafisa wa usalama katika kaunti watafuata. Tumeanza kujenga nyumba za muda zitakazotumiwa na maafisa hao tukisubiri kukamilishwa kwa nyumba za kudumu,” akaeleza.

Dkt Matiang’i alisema hayo alipozindua rasmi ujenzi wa nyumba katika kituo cha polisi cha Ol Moran.

Mradi huo wa ujenzi wa nyumba na majengo mengine ya kutumiwa na polisi, utafadhiliwa kwa pamoja na Serikali ya Kitaifa na ile ya Kaunti ya Laikipia.

“Utawala wangu umejitolea kuelekeza Sh20 milioni katika mradi huu. Utasaidia kuhakikisha uwepo wa polisi katika eneo hili na hivyo kuimarisha usalama,” akasema Gavana wa Laikipia, Ndiritu Muriithi ambaye aliandamana na Dkt Matiang’i.

Waziri pia alitangaza kuwa vituo vidogo vya polisi vya Luniyek na Survey vitapandishwa ngazi kuwa vituo vya polisi na maafisa zaidi kutumwa huko.

“Eneo hili la Laikipia linahitaji doria ya maafisa wa usalama zaidi kuliko hapo zamani,” Dkt Matiang’i akaeleza.

You can share this post!

KAMAU: Mapinduzi yanatoa dalili Afrika imeshindwa kujitawala

Wasichana 6 watimuliwa shuleni kwa mihadarati