Habari za Kitaifa

Serikali kukusanya maji ya mvua yatumike wakati wa kiangazi

May 5th, 2024 1 min read

NA LAWRENCE ONGARO

SERIKALI ina mpango wa kukusanya maji yote yanayotokana na mvua kubwa inayonyesha nchini ili kuyahifadhi kwa matumizi ya siku zijazo.

Katibu wa Idara ya Unyunyuziaji wa Maji Mashambani Ephantus Kimotho alisema hiyo ni njia bora ya kuhifadhi maji ili kuyatumia siku za kiangazi.

Alieleza kuwa tangu mvua kubwa ianze kunyesha, maji mengi yamepotea bure ambayo kama yangekusanywa na kuhifadhiwa kwa matumizi ya siku zijazo, ingekuwa ni faida kubwa katika uzalishaji wa chakula lakini pia kwa matumizi mengineyo.

Bw Kimotho alisema serikali ikichukua mwelekeo huo, bila shaka wakulima watapata maji mengi ya kunyunyizia kwenye mashamba yao huku pia mengine yakisafishwa kwa unywaji.

Katibu wa Idara ya Unyunyuziaji wa Maji Mashambani Ephantus Kimotho akihutubia wanahabari katika kijiji cha Magogoni. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Aliyasema hayo mnamo Ijumaa alipozuru kijiji cha Magogoni ili kunakoendeshwa mradi mpya wa maji wa takriban Sh400 milioni.

Kijiji cha Magogoni kiko Thika, Kaunti ya Kiambu.

Alisema kwa muda wa miaka 10, wakazi hao ambao wengi ni wakulima, wamekosa maji, hali inayoponza juhudi zao kupiga hatua katika kilimo.

Wakulima wapatao 1,500 watanufaika pakubwa na mradi huo utakapokamilika.

Bw Kimotho alisema matarajio ya serikali ni kuona wakulima hao wakipanua shughuli zao za kilimo huku wakinywa maji safi.

Katibu huyo alieleza tayari mradi huo umekamilika kwa kiwango cha asilimia 80 ambapo ni asilimia 20 iliyosalia kabla ya kukamilika kabisa.

Mkazi wa Magogoni, Bw Joseph Mwangi, alipongeza serikali kuu kwa kuwajali huku akisema kilimo kitaimarika pakubwa eneo hilo.

“Tumekuwa tukitatizika sana na ukosefu wa maji lakini hatua ya serikali kutuletea mradi wa maendeleo italeta mabadiliko makubwa,” alisema Bw Mwangi.

Katibu huyo aliandamana na mbunge wa Thika Bi Alice Ng’ang’a na viongozi wengine.

Bi Ng’ang’a atazuru tena eneo hilo ili kuhakikisha wakazi wananufaika na maji.