Habari Mseto

Serikali kukusanya taarifa za Wakenya wenye jinsia mbili

July 10th, 2018 1 min read

Mwakilishi Mwanamke wa Kaunti ya Kiambu Gathoni Wamuchomba(kulia) na Mwenyekiti wa Jopokazi linaloshughulikia sera na sheria za watu walio na jinsia mbili Bw Mbage Ng’ang’a wakihutubia wanahabari Julai 9, 2018.Picha/Evans Habil

Na LEONARD ONYANGO

SERIKALI imezindua shughuli ya kuhesabu na kukusanya taarifa kuhusiana na Wakenya waliozaliwa wakiwa na jinsia mbili; uume na uke.

Jopokazi linaloshughulikia sera na sheria za watu walio na jinsia mbili jana lilisema kuwa shughuli hiyo itaendeshwa katika kaunti zote 47.

Mwenyekiti wa jopokazi hilo Mbage Ng’ang’a alisema taarifa hizo zitakusanywa na maafisa 20 pamoja na watafiti watatu wa masuala ya kisheria.

“Maafisa hao watakutana na waathiriwa, wazazi au jamaa zao kwa lengo la kufahamu changamoto wanazopitia ili kubuni sheria itakayohakikisha kuwa hawabaguliwi na wanapata huduma sawa na Wakenya wengine wenye jinsia moja,” akasema Bw Ng’ang’a.

Jopokazi hilo liliundwa na afisi ya Mkuu wa Sheria mnamo Mei 2017 ili kukusanya data, kufanya utafiti na kutoa mapendekezo kuhusu sera na sheria itakayosaidia kulinda haki za watu waliozaliwa na jinsia mbili. Jopokazi hilo linatarajiwa kuwasilisha ripoti yake kwa Mkuu wa Sheria kufikia Oktoba mwaka huu.

“Tunawasihi watu walio na jinsia mbili, wazazi au jamaa zao pamoja na washikadau wengineo kujitokeza wakati wa shughuli hiyo ya ukusanyaji taarifa,” akasema.

Inakadiriwa kuwa asilimia 2 ya watu walizaliwa na jinsia mbili kote duniani.

“Humu nchini idadi ya watu walio na jinsia mbili haijulikani kwa sababu hakuna utafiti au taarifa zimewahi kukusanywa kuwahusu,” akasema Bw Ng’ang’a.

Watu waliozaliwa na jinsia mbili hukumbana na changamoto mbalimbali maishani kama vile unyanyapaa katika jamii na hata kutelekezwa na wazazi.

Kwa mfano, baadhi yao huonyesha dalili ya kuwa wasichana lakini wanapokuwa watu wazima umbile la kiume hujitokeza kwa wingi hivyo kubadilika kuwa wanaume. Hatua hiyo huwafanya kuwa na majina mawili yanayohusiana na jinsia ya kike na kiume.