Michezo

Serikali kulipa wanaspoti hadi corona idhibitiwe

April 23rd, 2020 1 min read

SERIKALI imeahidi kuwainua wanamichezo wa humu nchini kifedha hadi janga la virusi vya homa kali ya corona litakapodhibitiwa vilivyo.

Katika hotuba yake kwa taifa mnamo Jumatano, Rais Uhuru Kenyatta aliwahakikishia wanaspoti wote wa humu nchini kwamba serikali yake itasimama nao katika hali zote katika kipindi hiki kigumu ambapo shughuli zote za michezo, ambazo ni kitega-uchumi kwa familia nyingi, zimesimamishwa.

“Nawahakikishia wanamichezo wetu kwamba hatujawasahau. Tunajitahidi kadri ya uwezo wetu kubuni njia zitakazowawezesha kujikimu kimaisha. Serikali inafahamu ugumu mnaopitia katika kipindi hiki ambapo njia zenu za pekee za kujitafutia riziki zimeathiriwa pakubwa na ugonjwa huu hatari,” akatanguliza Rais Kenyatta.

“Tuna Hazina ya Kitaifa ya Michezo ambayo tutatumia kupata kiasi fulani cha fedha zitakazowafaidi wanamichezo wetu katika kipindi hiki. Tumejitolea kwa hali zote kuwafaa Wakenya wote ambao ukawaida wa maisha yao umetikiswa zaidi na janga hili. Tutaendelea kuwapa msaada hadi corona itakapodhibitiwa vilivyo,” akaongeza.

Hakikisho la Rais Kenyatta linatolewa siku moja tu baada ya Shirikisho la Soka la Kenya kufichua kwamba vinara wake wamekuwa wakijadiliana na Wizara ya Michezo kuhusu namna ya kuwasaidia wanasoka wa humu nchini wakati huu ambapo ulingo wa michezo umeathiriwa pakubwa kote duniani.

Sawa na michezo yote mingine, soka ambayo inajivunia idadi kubwa zaidi ya ushabiki ulimwenguni, pia ilisamimashwa huku tarehe rasmi za kurejelewa kwa mashindano mbalimbali zikisalia kizungumkuti.

Vikosi vyote vya michezo mbalimbali, vilitarajiwa jana Jumatano ya Aprili 22, kupitia kwa mashirikisho husika, kutoa orodha ya hadi wachezaji 30 ambao watanufaika na mpango mpya wa serikali wa kufaa wanaspoti kifedha.