Serikali kusaidia waajiri kuboresha maslahi na mazingira ya wafanyakazi

Serikali kusaidia waajiri kuboresha maslahi na mazingira ya wafanyakazi

Na SAMMY WAWERU

SERIKALI imetangaza kwamba itasaidia waajiri kuboresha mazingira ya wafanyakazi.

Katibu katika Wizara ya Utumishi wa Umma, Vijana na Jinsia, Bi Mary Kimonye alisema Jumatano serikali iko tayari kushirikiana na waajiri nchini kuimarisha maslahi ya wafanyakazi. “Serikali imejitolea kuhakikisha kila Mkenya ana bima ya afya.

Ninahimiza waajiri wakumbatia mpango huu ili kushusha gharama ya matibabu ya wafanyakazi wao,” Bi Kimonye akasema. Alisema hayo wakati akizindua rasmi kongamano la Usimamizi wa Wafanyakazi Nchini, linaloendelea Mjini Mombasa.

Kongamano hilo hata hivyo, lilianza Jumanne na linanuwia kujadili kwa mapana maslahi ya wafanyakazi nchini.Aidha, limehudhuriwa na vitengo vya kuajiri wafanyakazi kutoka kampuni, mashirika na idara  mbalimbali za serikali.

Mbali na kujadili maslahi ya wafanyakazi, pia linaangazia msongo wa mawazo, mazingira ya wafanyakazi, biashara na ajira. “Vitengo vya kuajiri vishirikiane na serikali ili tuboreshe maslahi na mazingira ya wafanyakazi, ikiwemo suala la likizo,” Katibu Kimonye akahimiza, wakati akihutubu.

Visa vya mauaji katika ndoa na kujitia kitanzi Kongamano hilo la 25 limejiri wakati ambapo visa vya wafanyakazi kujitia kitanzi kwa sababu ya hali ngumu ya maisha vinaonekana kuongezeka. Kwa mfano, katika Idara ya Kitaifa ya Polisi (NPS), baadhi ya maafisa wameripotiwa kujitia kitanzi, baada ya kuua wenzao kinyama kwa bunduki na hata raia.

Visa hivyo vinavyoegemea kwenye ndoa na uhusiano wa kimapenzi, vimetajwa kusababishwa na msongo wa mawazo unaochangiwa na ugumu wa maisha. Baada ya Kenya kuthibitisha kuwa mwenyeji wa Covid-19 mnamo Machi 2020, matukio hayo yameongezeka kwa kasi.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Utumishi wa Umma, Vijana na Jinsia, visa 5, 009 vya dhuluma za kijinsia (GBV) viliandikishwa kati ya Januari 2020 – Desemba 2020, kupitia nambari maalum ya 1195.

Come Together Widows and Orphans Organization (CTWOO) ni shirika lilisilo la kiserikali na linaloangazia masuala ya wajane na yatima, na takwimu zake zinaonyesha limeandikisha zaidi ya malalamishi 150 ya GBV kutoka kwa wanawake walio kwenye ndoa, tangu Machi 2020.

CTWOO inakiri hali ngumu ya maisha na kiuchumi inayochochewa na virusi vya corona imechangia ongezeko la visa hivyo. “Visa vya GBV vinazidi kuongezeka, hasa kwa sababu ya hali ngumu ya maisha. Ninahimiza wanandoa ndoa inaposhindikana kuna fursa ya talaka, kabla maji kuzidi unga.

Mauaji yanayohusishwa na ndoa na mahusiano ya kimapenzi yamekita mizizi,” Dianah Kamande HSC, mwanzilishi na Afisa Mkuu Mtendaji wa shirika hilo anaelezea. Hatua ya serikali kuahidi kushirikiana na waajiri kuboresha maslahi na mazingira ya wafanyakazi inajiri siku chache baada ya taifa kupoteza staa wa riadha duniani, Agnes Tirop, 25, kufuatia mzozo wa ndoa.

Septemba 2021, Dkt James Gakara aliyehudumu Nakuru aliua kinyama wanawe wawili na baadaye kujitia kitanzi katika kile kilitajwa kama kusababishwa na msongo wa mawazo.

You can share this post!

IEBC yaeleza wasiwasi kuhusu idadi ya chini ya...

Inasikitisha ni wahudumu 10 pekee wa afya wamefuzu...

T L