Serikali kusaka wanaorai wasichana wa shule kushiriki biashara ya ngono

Serikali kusaka wanaorai wasichana wa shule kushiriki biashara ya ngono

NA MWANGI MUIRURI

SERIKALI imeahidi kuanzisha msako mkali dhidi ya mashirika ya mabwenyenye, kijamii na kiuchumi yanayowalaghai wasichana wa shule kujiunga na biashara ya ngono mjini Makutano.

Mji huo unapakana na Kaunti za Embu na Kirinyaga kwenye makutano ya barabara inayoelekea Nyeri na Nanyuki kupitia Sagana na Meru kupitia Ngurubani.

Ni mji wa kipekee ulio mwendo mfupi kutoka kaunti za Murang’a na Machakos hivyo kuufanya kituo kikuu ambapo wanajamii kutoka Mlima Kenya hukutana kwa biashara hiyo ya kuchuuza miili yao.

Barua ya malalamishi iliyoandikiwa Kamati ya Ulinzi Kaunti ya Embu na Muungano wa Kutetea Maslahi ya Wafanyabiashara kwa Wakazi wa Makutano inasema “haya sasa yamepita mipaka na hatuwezi kuendelea kuwa mashabiki wa dhuluma za watoto zinazofanyika hapa.”

Wakazi hao wamefichua kuwa wasichana wanaofurika mjini humo kushiriki biashara ya ngono ya watoto hasa wanatoka kaunti za Murang’a, Machakos, Nyeri, Embu na Kirinyaga huku wachache wakitoka kaunti za Kiambu na Meru.

“Wasichana hao huacha shule, wanatoroka makwao na kuishi mjini humu ili kuanza maisha yao kama wachuuzi wa ngono na kwenye harakati hizo wananaswa kwenye mitandao ya wahalifu sugu,” ilisema barua hiyo.

Aidha, wamefichua kuwa wasichana hao hukumbana na kila aina ya dhuluma kutoka kwa wakubwa wao huku majambazi wa mitaa hiyo na maafisa wa polisi waovu wakiitisha huduma za bure kama njia ya kuwapa mafunzo na kukubalika mjini huko.

“Licha ya wakazi eneo hilo kutoa taarifa kwa maafisa wakuu na viongozi wa ulinzi kupitia jumbe za siri, kudokezea vyombo vya habari na kuwasilisha malalamishi kwa usimamizi eneo hilo, hakuna chochote kinachofanywa,” wanalalamika.

Taswira ya mji huo ni pesa za harakaharaka mikononi mwa mawakala wa kilimo, wacheza kamari, walanguzi wa mihadarati na pombe haramu ikiwemo mashirika yanayoendesha hadharani biashara ya mafuta ya magendo.

“Tumejaribu kadri tunavyoweza kupiga vita hali hii ya kutamausha… ni uchungu mno kuwaona wasichana wakiwasili mjii huu wakiwa wamevalia sare ya shule, wanajiandikisha wenyewe kwenye madanguro na kuanza maisha kama wachuuzi wachanga wa ngono,” alisema mzee wa Kanisa la Anglikana Joseph Muinde.

Kamishna wa eneo hilo anayeondoka Evans Achoki ni miongoni mwa waliopokea katika muda wa miezi mitatu iliyopita, vidokezo kuhusu uozo unaoendelea katika mji huo mdogo.

“Naam, nilifahamishwa. Nimekuwa nikijadili suala hilo na timu zilizo mashinani na hatua itafuatia,” alisema.

Huku hatua ikiendelea kucheleweshwa, wazazi waliofadhaika wanazidi kumiminika mjini humo kuwasaka binti zao wapotovu walionaswa kwenye biashara ya ngono, mihadarati, uchezaji kamari na ulanguzi wa mafuta.

“Nimekuja mara tatu katika mji huu kumtafuta binti yangu aliyeachia shule Kidato cha Pili kutoka eneo la Murang’a Kusini,” anasimulia Bi Jacinta Mueni.

  • Tags

You can share this post!

Magoha kuzikwa Februari 11 kwake Gem

Mashemeji Derby yaishia sare Nairobi City Stars ikigomea...

T L